Patachimbika Coastal, Azam Mkwakwani leo

14Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Patachimbika Coastal, Azam Mkwakwani leo

KIVUMBI cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kinatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya wenyeji Coastal Union dhidi ya Azam FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

WACHEZAJI WA COASTAL UNION

Azam FC inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuongeza kasi katika mbio za ubingwa, ambako inakimbizana na vigogo Yanga SC na Simba SC kileleni, wakati Coastal inahitaji ushindi ili kujiondoa kwenye maeneo ya hatari kuelekea kushuka daraja.

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Ally Jangalu, amesema kwamba atahakikisha timu yake inashinda mchezo huo ili wapate pointi tatu muhimu. Jangalu ameema wanaiheshimu Azam FC kwa sababu ni timu bora na watahakikisha wanautumia vyema Uwanja wao Mkwakwani leo ili washinde.

“Tumejiandaa vyema na hatuna mchezaji majeruhi, tunamuomba Mungu atujaalie tushinde mchezo wetu ili tujiimarishe kwenye msimamo kwa kuwa hatuko kwenye nafasi nzuri,” alisema Jangalu.

Kwa upande wake, kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amesema wanataka ushindi katika mchezo huo ili kuendelza rekodi yao nzuri ya kutofungwa kwenye mechi za ugenini.

Hadi sasa, Azam FC imecheza mechi saba ugenini, ikishinda sita na kutoa sare mchezo mmoja dhidi ya Yanga (1-1) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kitakwimu imekusanya pointi 19 ugenini kati ya 21 ilizotakiwa kuzipata.

Coastal Union iliyojikusanyia jumla ya 13 katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, mabao yaliyofungwa na Shomari Kapombe na Kipre Tchetche.

Hall amesema anajua mchezo huo utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kushinda, huku akisisitiza kuwa wana rekodi nzuri ya ushindi katika Uwanja wa Mkwakwani, mjini Tanga wanakoenda kuchezea.

Coastal Union wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa 2-1 na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, wakati Azam FC ilishinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Azam, Complex, Chamazi, Dar es Salaam.