Wiki iliyopita timu hizo zote zilitoa sare kwenye mechi zao zilizocheza.
Kitayosce, ikiwa nyumbani, Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora iliifunga Mbuni FC bao 1-0, lililowekwa ndani ya wavu dakika ya sita tu ya mchezo na straika Mkongomani, Fabrice Ngoy wa Ngoy ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo.
Matokeo hayo yanaifanya Kitayosce kubakisha mechi moja tu kabla ya kuhitimisha mechi zake kwenye Ligi ya Championship ikishika nafasi ya pili kwa pointi 57, chini ya JKT Tanzania ambayo tayari imeshamaliza mechi zake na imepanda Ligi Kuu ikiwa na pointi 63.
Pamba ikiwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na kuendelea kung'ang'ania nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi ya Championship kwa pointi 56, moja nyuma ya Kitayosce. Bao pekee la washindi lilifungwa dakika nane kabla mechi kumalizika na William Kisingi.
Timu zote hizo mbili zimebakisha mechi moja na atakayemaliza nafasi ya pili ataungana na JKT Tanzania kupanda moja kwa moja na itakayobaki itakwenda kucheza mechi za mchujo na timu za Ligi Kuu.
Wakati huo huo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imepokea barua ya maombi kutoka klabu ya Ndanda ya mkoani Mtwara wakiwasilisha maombi yao ya kujitoa kwenye Ligi ya Championship msimu wa 2022/23 kwa kile walichoeleza kuwa ni kutokana na changamoto ya kifedha.
Klabu hiyo ilishindwa kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mechi namba 230 ya Ligi ya Championship dhidi ya Pan African uliopangwa kucheza Mei 6 kwenye Uwanja wa Uhuru.
Kwa maelezo hayo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inatangaza kuwa mchezo huo hautokuwapo na taarifa itapelekwa kwenye Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kwa ajili ya kujadiliwa, kisha kutolewa maamuzi.










