Simba itawakaribisha Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 waliyopata katika mechi ya mzunguko wa kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa Oktoba 23, mwaka jana.
Mnyama anahitaji kuvunja mwiko wa kutopata ushindi katika mechi saba mfululizo huku Yanga wakitaka kuendelea kusaka pointi tatu wakiwa wamecheza michezo 22 bila ya kupoteza na kujihakikisha ubingwa wa msimu huu.
Timu hizo zinakutana zikiwa na utofauti wa alama nane, Yanga ambao ni mabingwa watetezi wakiwa kileleni na pointi 68 kibindoni huku Simba yenye pointi 60 ikifuatia.
Kuelekea mechi hiyo ya dabi, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho' amesema anajivunia ubora wa safu yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikifanya vizuri chini ya uongozi wa Jean Baleke, ambaye leo atakuwa anacheza mchezo wa kwanza dhidi ya watani zao.
Robertinho alisema maadalizi ya mchezo huo yapo vizuri na anaamini watafanya vizuri katika mechi hiyo ili kuhakikisha wanajiweka sehemu salama kuelekea kwenye mbio za ubingwa.
Kocha huyo alisema wamejiandaa kufanya vizuri na wanatambua endapo watafungwa katika mchezo huo, tayari watawapa ubingwa wapinzani wao jambo ambalo hawapo tayari kuona linatokea.
“Simba hatutaenda kubadili aina yetu ya uchezaji kwa sababu mechi ya Yanga ni kama mechi nyingine tu, wachezaji wana morali na wanautaka mchezo. Malengo yetu ni kucheza vizuri na kushinda. Tuna Baleke (Jean), sasa tunajivunia sana, Mohammed Hussein, Shomari (Kapombe) wana uwezo mkubwa, nimezungumza na wachezaji wameniahidi kufanya vyema kesho (leo) , tunawaheshimu Yanga," alisema Robertinho.
Aliongeza lengo la Simba ni kubeba pointi tatu za mechi hiyo huku wakiingia uwanjani wakifahamu vizuri wapinzani wao na amewalekeza nyota wake kucheza soka litakalowafurahisha mashabiki wao.
Nahodha Msaidizi wa Simba, Hussein, alisema benchi la ufundi limemaliza kazi yake na wao kama wachezaji wamepokea walichofundishwa mazoezini na sasa wanakwenda kukamilisha mchezo.
“Tunatambua tukifungwa tunawapa ubingwa wenzetu na sisi hatupo tayari kuwapa ubingwa kwa kuwa tunautamani, tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema beki huyo.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, alisema mechi hiyo ni kubwa na si kwa Afrika Mashariki tu, bali ni Afrika nzima, hivyo hawatakuwa tayari kupoteza mbele ya mashabiki zaidi ya 50,000.
Kaze alisema wanaingia uwanjani bila presha na anaamini wapinzani wao ndio wana wasiwasi kwa sababu wakipoteza watawapa nafasi kubwa ya kutangaza ubingwa.
Kuhusu kiwango cha mshambuliaji wao tegemeo, Fiston Mayele, alisema ubora wa nyota huyo ni mkubwa na si uwanjani tu, hata anapokuwa na wenzake anawahamasisha wawe na hali ya kujiamini ili kufanya vizuri.
“Kikosi cha Simba kipo vizuri katika safu ya ushambuliaji lakini kwa kuwa tunacheza kama timu, ninaimani tunaweza kuwazuia kutopata nafasi ya kufunga,” alisema Kaze.
Aliahidi kikosi chake kimejipanga kutoa burudani stahiki kwa mashabiki na wanachama wao kwa kiwango kizuri ili kupata matokeo bora yatakayowapeleka kwenye malengo.
“Tumejiandaa kucheza kama timu yaani tutalinda kama timu mpaka kushambulia kama timu kwa utulivu na umakini mkubwa sana ili kupata pointi tatu muhimu katika hii dabi," Kaze alisema.
Mudathir Yahya, kiungo wa Yanga, alisema wapo tayari kwa mapambano na wamejiandaa kufanya vizuri katika mechi hiyo.
“Hatuna presha, tunautaka ubingwa na tukishinda katika mchezo huo tunakuwa mabingwa, tupo vizuri na tutaendelea kuwa bora na tunaamini itakuwa dabi ngumu kwa kuwa ndio tutatakiwa kutangaza ubingwa mbele ya mpinzani,” alisema Mzanzibari huyo.










