Kwa mujibu wa takwimu za Ligi Kuu, Mayele, straika wa Yanga anaendelea kuongoza katika orodha ya wafungaji akiwaacha wenzake kwa mbali baada ya Jumanne iliyopita kufikisha mabao 16.
Kwenye eneo la kutoa pasi za mwisho za mabao 'assist', Chama wa Simba bado ni mfalme akiwa ametoa pasi 14 zilizozaa mabao, akiwaacha wengine maili nyingi.
Kipa wa Yanga, Diarra ni kinara wa kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao 'clean sheets' Jumanne iliyopita dhidi ya Kagera Sugar akitimiza mechi 15, huku kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza, akiwa ndiye mchezaji aliyechangia mabao mengi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa, yaani ya kufunga yeye mwenyewe na yale aliyotoa pasi za mwisho.
Ntibanzokiza, raia wa Burundi amepachika mabao 10 mpaka sasa, sita akiyafunga akiwa Geita Gold na manne akiwa Simba, akiwa pia na 'assist' tisa, hivyo kuwa na mchango wa mabao 19.
Wakati Mkongomani Mayele ana mabao 16, Saido na Moses Phiri wote wa Simba wana mabao 10 kila mmoja, Bruno Gomes wa Singida Big Stars, John Bocco wa Simba na Sixtus Sabilo wa Mbeya City, wote kila mmoja akifunga mabao tisa.
Wakati Mzambia Chama anatamba na 'assist' zake, anafuatiwa na Saido mwenye tisa, Ayoub Lyanga wa Azam akiwa nazo saba, Sabilo wa Mbeya City na Nicolaus Gyan wa Singida Big Stars wakiwa 'assist' sita kila mmoja huku Ally Ramadhani 'Kagawa' wa Kagera Sugar, Deus Kaseke wa Singida Big Stars, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin na Mohames Hussein 'Tshabalala' wote wa Simba na Shiza Kichuya wa Namungo wote hao wakiwa na 'assist' tano kila mmoja.
Katika eneo la 'clean sheets', baada ya Diarra golikipa anayefuatia ni Aishi Manula wa Simba (12), Ally Ahmada wa Azam FC (8), Metacha Mnata wa Yanga (7), Mahmoud Mroivil wa Coastal Union, Fikirini Bakari wa Ihefu na Said Kipao wa Kagera Sugar kila mmoja ana 'clean sheets' tano.










