MTAKOMA Yanga kama faru aliyechokozwa leo

03Feb 2016
WAANDISHI WETU
Lete Raha
MTAKOMA Yanga kama faru aliyechokozwa leo

KIVUMBI cha Ligi Kuu Tanzania Bara kitaendelea leo kwenye viwanja saba huku mchezo kati ya Yanga na Prisons kwenye uwanja wa Sokoine ukitajwa kuwa ndiyo unaosubiriwa kwa hamu baada ya mabingwa hao kulala 2-0 dhidi ya Coastal Union wikiendi iliyopita.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, aliwasili jana Mbeya akifuatana Kamati ya Mashindano, chini ya Mwenyekiti Isaac Chanji, kwa lengo la kuhakikisha timu inapata hamasa na kushinda leo.
Katika mzunguko wa kwanza kwenye uwanja wa Taifa, Yanga waliilaza Prisons 3-0, mabao yaliyofungwa na Mbuyu Twite, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
Katika mchezo wa leo, Yanga watamkosa beki wao, Kelvin Yondani, anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal. Yanga pia wataendelea kumkosa nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na beki wa kushoto Haji Mwinyi ambao ni majeruhi.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, huenda akawaanzisha kwenye safu ya ulinzi ya kati mabeki Vicent Bossou na Mbuyu Twite.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, alisema baada ya kupoteza mchezo uliopita, wameelekeza nguvu kwenye mechi ya leo ili kuendeleza kampeni yao ya kuutetea vyema ubingwa wao.
“Kushindwa dhidi ya Coastal imebaki kuwa historia, sisi tunaangalia mbele na Prison lazima wakione kwani tunataka kuendelea kuwa kileleni,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo, Prisons wanawangoja Yanga kwa hamu baada ya maandalizi ya kutisha kufuatia kuahirishwa kwa mechi yao dhidi ya Azam iliyoenda katika michuano maalum nchini Zambia.
Kocha wa Prisons, Salum Mayanga alisema, "Nimekipanga vyema kikosi changu kwa ajili ya mzunguko wa pili kuhakikisha hatupotezi mechi. Lengo ni kuona timu yangu inapata matokeo mazuri. Tuko tayari kuikabili Yanga na ninaamini tunaweza kufanikiwa kuwafunga kwenye mechi hii.”

Simba v Mgambo
Mchezo mwingine unaosubiriwa kwa hamu ni ule wa Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam pale Simba itakapowakaribisha Mgambo JKT.
Mgambo itakuwa ikipigania kulipa kisasi baada ya kulala 2-0 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza Mkwakwani, Tanga.
Simba itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa magoli 4-0 walioupata Jumamosi dhidi ya African Sports, huku straika Hamisi Kiiza akiongeza kasi yake ya kufunga na kumpa presha kinara wa mabao wa ligi kuu, Amissi Tambwe wa Yanga.
Mgambo wao wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya goli 1-1 dhidi ya Ndanda FC kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakiwa nafasi ya tisa baada ya kujikusanyia pointi 17.
Kocha wa Mgambo, Bakari Shime, alisema mechi itakuwa ngumu, lakini wamejipanga kuondoka na pointi tatu leo.
Kwa upande wake, kocha wa Simba, Jackson Mayanja, alisema anaamini vijana wake wameanza kumuelewa na hivyo anaamini wataendelea kufuata kile anachowaelekeza.
Alisema kuwa anatarajia kuwatumia washambuliaji Danny Lyanga na Paul Kiongera ambao wamerejea uwanjani baada ya kupona majeraha.

MECHI NYINGINE
Kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Kagera Sugar wataikaribisha Majimaji, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Mbeya City, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga African Sports wataikaribisha Mwadui FC wakati Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Toto Africans kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Kesho ligi itaendelea kwa mchezo mmoja kati ya Coastal Union na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Hata hivyo, mechi kati ya Azam na Stand United iliyokuwa ichezwe leo haitakuwapo kwani Azam wako ziarani Zambia.

*Imeandaliwa na Bakari Kagoma na Victor Ndunguru