Akizungumza katika hafla maalumu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula, alisema anawashukuru MobiAd Africa kwa udhamini huo kwa sababu kanuni ya mafanikio siku zote lazima iwe na mwanzo.
“Simba inakwenda mbele kutambua vipaji na kuvichukua, kuviendeleza na kutengeneza timu yenye vipaji vikubwa sana, tunaamini Simba imara yenye vipaji haitaisaidia Simba pekee bali hata taifa letu," alisema Kajula.
Aliongeza kanuni ya mafanikio ya kila kitu lazima kianzie mwanzo, Simba wameona umuhimu wake wamerudi kwenye njia zao za zamani na kutamba wanaongoza kutoa wanaocheza kwa mkopo katika timu nyingine za Ligi Kuu Bara na za daraja la kwanza.
"Ni safari ndefu ambayo inahitaji mshikamano tuna mategemeo chanya huu ni mwanzo tu kuna udhamini mkubwa unakuja tumeamua kufanya kazi na Simba ni timu kubwa barani Afrika ambayo iko mstari wa mbele katika kukuza soka la vijana.
Tunataka kuondoa bahati kwenye mpira na tunataka kuwaandaa vijana wenye vipaji ili baadaye kuja kuisaidia timu na vijana watakaopatikana tutawasomesha Simba wenyewe," alisema Kajula.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa MobiAd Africa, Lumisho Sikoni, alisema anaishukuru Simba kwa kuwapa nafasi ya kufanya nao kazi kwa sababu wanafahamu vijana ni taifa la kesho hivyo matayarisho yao yanapaswa kuanza leo.
“Ni safari ndefu ambayo inahitaji mshikamano, tumeamua kufanya kazi na Simba, ni timu kubwa barani Afrika ambayo iko mstari wa mbele katika kukuza soka la vijana,” alisema Sikoni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah “Try Again’ naye aliishukuru kampuni hiyo na kuongeza mazungumzo ya kufanikisha udhamini huo hayakuwa rahisi.
“Hakuna miujiza kwenye soka ili kupata timu nzuri unapaswa kuwekeza kwa vijana, tunaamini pesa hizi zitatimiza malengo yenu na yetu, Simba ina malengo ya kuchochea soka la vijana,” alisema Try Again.










