Geita Gold itawafuata Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi iliyopita ya mzunguko wa pili Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kulazimisha sare katika mchezo wa kwanza.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Geita Gold, Mathius Wandiba, alisema wanawaandaa wachezaji wao kiufundi na kisaikolojia kwa sababu wanahitaji kushinda na kusonga mbele katika michuano hiyo.
Wandiba alisema anafurahi kuona ushindani ni mkubwa katika mazoezi ya timu hiyo huku nyota hao wakijiimarisha kimwili.
"Tumewaandaa wachezaji wetu vizuri kuelekea katika mchezo huo, tunafahamu utakuwa mgumu na wenye ushindani, tunajiwinda ili kutimiza lengo la kuingia hatua ya nusu fainali," alisema Wandiba.
Kocha huyo alisema makosa ambayo waliyaona katika michezo iliyopita wanaendelea kuyafanyia marekebisho na kuwasisitiza wachezaji kuongeza umakini wanapokaribia lango la wapinzani.
Alisema hawahofii kukutana na Yanga ambayo itaingia katika mechi hiyo ikiwa na rekodi ya matokeo bora kwenye michezo yake ya kimataifa ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
"Hatuna wasi wasi kukutana na Yanga, kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa si kigezo cha kuwaogopa, hii ni michuano mingine ambayo ina mbinu na kanuni tofauti," Wandiba aliongeza.
Amewataka mashabiki wao waliopo Dar es Salaam kujipanga kujitokeza kuwashangilia kwa sababu wamepanga kutimiza malengo yao ya kushiriki michuano ya kimataifa katika msimu ujao.










