Mkwasa: Stars tutashambulia

03Jun 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Mkwasa: Stars tutashambulia

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Boniface Mkwasa amesema amekiandaa kikosi chake kucheza soka la kushambulia muda wote katika mechi yao dhidi ya Misri itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Boniface Mkwasa

Stars itawakaribisha Misri katika mechi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za mwakani za Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya mechi hiyo Septemba itaifuata Nigeria.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa alisema kuwa atawatumia zaidi viungo kwa ajili ya kufanya mashambulizi badala ya kuzuia ili kusaka goli mapema katika mchezo huo wa tatu wa Kundi G.

“Hiyo ndiyo mipango yangu katika mchezo huo, naamini goli la mapema litawachanganya wapinzani wetu na hivyo tutakuwa tumejiweka katika mazingira mazuri ya kupata ushindi, ” alisema Mkwasa.

Alisema matokeo ya ushindi ndiyo kitu pekee wanachokihitaji katika mechi hiyo ili kufufua matumaini ya Tanzania kufuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika Gabon mwakani.

Aliongeza kuwa anafahamu ubora wa wapinzani wao lakini lazima timu yake ipambane na kupata ushindi ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

“Mazingira ya kundi letu ni lazima tushinde mchezo wa Jumamosi kabla ya kuufikiria mchezo mwingine, na wachezaji wanafahamu hilo,” Mkwasa alisema.