Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, Mkwasa alisema kuwa bado hafahamu mustakabali wake na timu hiyo baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Misri na kuzima 'ndoto' za kufuzu michuano hiyo itakayofanyika nchini Gabon.
Mkwasa alisema kuwa mechi ya mwisho itakayofanyika Septemba dhidi ya Nigeria, haitakuwa na ushindani kutokana na timu zote kupoteza nafasi ya kwenda kwenye fainali hizo.
"Ukweli bado ninaugulia yale matokeo, kila nikikumbuka inasumbua akili yangu, siwezi kusema mengi, pia sielewi nini kitafuata," alisema Mkwasa.
Kocha huyo wa zamani wa Twiga Stars, Ruvu Shooting na Yanga alisema kama ingekuwa ni mapenzi yake, angeomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wenzao wa Nigeria waiombe CAF ili mchezo huo usifanyike kwa sababu hauna faida kwa pande zote mbili.
Misri ilifuzu fainali hizo kutoka Kundi G baada ya kufikishia pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na Nigeria na Tanzania zenye pointi moja kila moja. Chad iliyokuwa kwenye kundi hilo ilijitoa mapema kwenye mashindano hayo.










