Yanga iko Kundi A, na mchezo wake wa kwanza wataifuata Mouloudia Olympique Bejaia (Mo Bejaia) Juni 17, mwaka huu.
Katika kundi hilo, pia wamo TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC na Medeama kutoka Ghana.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema hadi sasa bado hawajafahamu kama timu itakwenda nje ya nchi au itabaki kujiandaa nyumbani.
Lakini kiongozi mmoja wa Yanga (jina linahifadhiwa), alisema mipango ya timu hiyo kwenda kuweka kambi nje ya nchi kama ilivyoelezwa awali, haipo tena.
"Tuko kwenye majadiliano, hatujaamua waki timu itakwenda kuweka kambi. Kuna mambo mengi lazima tuyaangalie kabla ya kuamua," alisema Pluijm.
Aliongeza: "Kuna mambo mengi yako katika programu yangu, lakini bado uongozi haujaamua."
Wakati huohuo, wachezaji wa kigeni wote wameshawasili kutoka katika nchi zao isipokuwa beki wake wa kati, Vicent Bossou kutoka Togo.
"Bossou tu ndio hajafika, tunatarajia kumpokea kesho (leo), ila Haruna (Niyonzima), Tambwe (Amissi), Donald Ngoma na Kamusoko (Thaban) wao wapo nchini tayari," alisema meneja wa Yanga, Hafidh Saleh.
Kikosi cha Yanga kilianza mazoezi jana jioni kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.










