Mgosi airudishia Simba ubingwa

24Apr 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Mgosi airudishia Simba ubingwa

NAHODHA wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’, amesema kuwa ameangalia hali ya wachezaji wenzake na idadi ya mechi zilizobaki kwenye ligi akisema kutwaa ubingwa inawezekana.

MGOSI

Mgosi alisema kuwa hataki kuingia kwenye vita ya maneno, lakini akadai wingi wa mechi mfululizo waliopitia Yanga unaweza kuwachosha na kuwafungulia njia ya ubingwa Simba.

“Ni ngumu kucheza michuano ya kimataifa, na kwenye ligi na makombe mengine nyumbani kwako ukafanya vizuri. Kama Yanga wataweka nguvu kubwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, naamini pointi 18 kwenye mechi sita walizobaki nazo watazikosa.

“Kama wakiteleza kwenye mechi mbili tu, tunaweza kuwapoteza. Kinachotakiwa kwetu ni kupambana mpaka dakika ya mwisho wa ligi msimu huu kwani lolote linaweza kutokea na sisi tukawa mabingwa,” alisema straika huyo.

Katika hatua nyingine, beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, alisema, “Simba haijaamua kufanya vizuri. Wakiwa tayari wanaweza kutwaa ubingwa, lakini wakiendeleza siasa ambazo haziwasaidii, hakika watapotea.”