Mfukuzano wakolea Simba, Yanga

03Feb 2016
Nipashe
Mfukuzano wakolea Simba, Yanga
  • ***Duru la lala salama ligi kuu linaingia raundi ya pili, huku mabingwa watetezi wakiwa Mbeya na Msimbazi wakibaki Dar...

MABINGWA Yanga walipoteza mechi yao ya kwanza msimu huu, huku mahasimu wao, Simba wakishinda mechi ya tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara na leo vigogo hao wanashuka dimbani Mbeya na Dar es Salaam kuendelea na hesabu za kusaka taji.

MABINGWA Yanga walipoteza mechi yao ya kwanza msimu huu, huku mahasimu wao, Simba wakishinda mechi ya tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara na leo vigogo hao wanashuka dimbani Mbeya na Dar es Salaam kuendelea na hesabu za kusaka taji.
Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kujaribu kutibu majeraha ya kipigo cha kushtukiza walichokipata kutoka Coastal Union ya Yanga wiki iliyopita.
Simba chini ya kocha Jackson Mayanja iko nyuma pointi tatu kuikuta Yanga yenye pointi 39 baada ya kushinda mechi tatu mfululizo na leo wanakipiga na Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Taifa.
Kocha wa Yanga, Hans Van der Pluijm alisema kipigo walichopata kutoka Coastal kiliwashtua, lakini pia kimewapa funzo muhimu wakati ligi ikigusa duru la lala salama.
Kocha huyo alisema sasa hawana namna tena zaidi ya ushindi kwenye mechi zote zinazofuata.
Pluijm anajigamba hivyo, huku akiwa na upungufu kwenye safu yake ya ulinzi itakayowakosa mabeki wawili mahiri.
Nahodha Nadir Haroub bado majeruhi na Kelvin Yondan hatakuwepo uwanjani kutokana na kuonyesha kadi nyekundu mechi dhidi ya Union.
Katika kuhakikisha wanashinda mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu, Pluijm sasa atamtumia Rajab Zahir na Vicent Bousou kucheza nafasi ya ulinzi.
Yanga ilipoteza mechi yake ya mwisho Ligi Kuu Bara Mei mwaka jana na anakutana na Prisons iliyo katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 27.
Beki Mbuyu Twite alisema watacheza mechi ya leo wakijua matokeo yoyote nje ya ushindi yatawapa nafasi wapinzani wao katika mbio za ubingwa.
"Mechi itakuwa ngumu, tunacheza katika mazingira ambayo ni lazima tushinde ili siyo tu kujiweka kwenye nafasi nzuri, bali bali kurejesha imani kwa mashabiki wetu," alisema Twite.
Kocha wa Simba, Mayanja amesema wazi kuwa pamoja na kikosi chake kuendelea kufanya vizuri baada ya kushinda mechi tatu mfululizo, lakini aamini bado hajakata kiu ya mashabiki wa Simba.
Alisema mashabiki wa Simba wana kiu ya ubingwa, hivyo ushindi mfululizo wanaoupata utamaliza kiu pale watakapotaa ubingwa baada ya muda mrefu.
"Nimewaambia wachezaji wangu kwamba hakuna mechi ya kudharau -- hakuna mechi rahisi wala timu ndogo," alisema Mayanja na na kuongeza: "Hatuwezi kwenda uwanjani tukiwa na nadharia kama tayari tuna matokeo ya ushindi mkononi. Tunacheza ligi yenye timu ngumu na zisizotabirika.
Mbali na mechi hizo za vigogo, pia ligi itasugua nyasi kwenye viwanja kadhaa, huku Kagera Sugar wakiwa nyumbani kuivaa Majimaji ya Songea.
African Sports inayoburuza mkia baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya 16, itakuwa nyumbani Mkwakwani kuikaribisha Mwadui.
Kadhalika, Ruvu JKT nao wataisubiri nyumbani Mbeya City iliyo nafasi ya 10 kwenye msimamo na kesho wababe wa Yanga, Coastal Union wataumana na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani.