Mshindi mara nane wa tuzo ya Ballon d'Or Messi alicheza misimu miwili na Mbappe katika klabu ya PSG kabla ya kujiunga na Inter Miami kama mchezaji huru Julai 2023.
Wakati wakiwa pamoja, Mbappe na Messi walishinda mataji mawili ya ligi na moja la Coupe de France ingawa Messi na mchezaji mwenza Neymar walizomewa katika miezi yao ya mwisho katika klabu hiyo baada ya kutolewa mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora.
"Mara zote utamisi kucheza na Leo Messi," alisema Mbappe akiiambia Amazon Prime Sport.
"Kwa fowadi kama mimi, unapenda kukimbia mbele, ukiwa naye katika timu yako una uhakika unaweza kupata mpira.
“Kwa ujumla, kucheza naye, imekuwa maalum. Messi anastahili heshima zote na kwa kweli nchini Ufaransa, hakupata heshima aliyostahili."
Mbappe, ambaye alifunga Jumatano na kuisaidia PSG kutwaa Kombe la Ufaransa, alisema baada ya mechi hiyo kuwa bado hajafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia na Ufaransa analengwa kwa muda mrefu na Real Madrid na mkataba wake na PSG unamalizika msimu huu wa joto.
"Bado sijafanya uamuzi wangu," alisema Mbappe akiwaambia waandishi wa habari. "Sijafanya chaguo”.
"Lakini kama nilivyosema, muhimu zaidi ni mataji. Tumeshinda moja tayari na tumedhamiria kushinda zaidi."
Mbappe mwenye umri wa miaka 25, alikuwa karibu kujiunga na Madrid msimu wa joto wa 2022 kabla ya kutangaza kubakia Parc des Princes.
Mbappé, ambaye alisajiliwa kutoka Monaco mwaka 2017 ndiye mfungaji bora wa muda wote wa PSG, ameshinda mataji matano ya Ligue 1 akiwa na klabu hiyo.
PSG wanaongoza Ligue 1 kwa pointi tano na watamenyana na Real Sociedad katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa.









