Kwa mujibu wa takwimu zetu za zile zilizotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Nchini (TPLB), Aziz Ki amefunga mabao matatu kwa mipira ya faulo hadi kufikia raundi ya 14 ya ligi hiyo, huku kukiwa hakuna mchezaji yoyote ukiondoa yeye aliyefunga mabao hata mawili kwa njia hiyo.
Takwimu za Nipashe zinaonyesha Aziz Ki alifanya hivyo katika mechi dhidi ya JKT Tanzania, Yanga ikishinda mabao 5-0, dhidi ya Azam FC, akiiongoza timu yake kupata ushindi wa magoli 3-2 na dhidi ya Tabora United, Yanga ikivuna pointi tatu kwa ushindi wa goli 1-0.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa msimu uliopita akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast ameendelea kujiwekea rekodi nyingi nzuri mpaka sasa, akiwa ndiye kinara anayeongoza kwa upachikaji wa mabao mpaka sasa, akiwa na magoli 10, akiwa pia mmoja wa wachezaji wanaoongoza kwa usaidizi wa mabao.
Nyota huyo ameisaidia timu yake kupatikana kwa mabao 12 kutokana na 'assist' zake mbili na kwenye rekodi hiyo yupo sawa na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC.
Kiungo huyo mwenye mashuti makali pia ndiye mchezaji anayeongoza kwa kufunga mabao mengi kwa mguu wa kushoto mpaka sasa, akiwa amepachika mabao nane.
Takwimu zinaonyesha baada ya Aziz Ki, wachezaji waliobaki wote wamefunga faulo moja kila mmoja.
Wachezaji hao ni Cheikh Sidibe wa Azam FC, Disan Galiwango (Kagera Sugar), Martin Kigi (JKT Tanzania), Ibrahim Ajibu (Coastal Union), Velentino Mashaka (Geita Gold FC), Omari Kindamba (Mashujaa FC), Marouf Tchakei na Gadiel Michael (Singida Fountain Gate) na Edwin Balua wa Tanzania Prisons.