Mayanja: Nina mechi 10, tulieni

26Feb 2016
Dar
Nipashe
Mayanja: Nina mechi 10, tulieni

BAADA ya kupoteza mechi wikiendi iliyopita dhidi ya Yanga kwa mabao 2-0, kocha wa Simba, Jackson Mayanja amewataka wachezaji, mashabiki na viongozi wa timu hiyo kusahau kipigo walichopata na wasubiri ushindi katika mechi 10 zijazo za Ligi Kuu.

kocha wa Simba, Jackson Mayanja.

Raia huyo wa Uganda alisema: “Soka lina matokeo matatu; kushinda, kupoteza na kutoka sare. Tumepoteza mchezo dhidi ya Yanga. Hatupaswi kuwaza kipigo hicho, tuna mechi 10 za ligi mbele yetu na michezo ya Kombe la Shirikisho."

“Kama tutapata pointi 30 katika michezo 10 ijayo, nina uhakika ubingwa unaweza kutua msimbazi kwa kufikisha pointi 85, ambazo huenda zisifikiwe na klabu nyingine.

“Naamini kuteleza kwa Yanga si mwisho wa kila kitu, tutatwaa ubingwa kwa kupambana na kuwa na umoja ndani ya klabu.
“Kiufundi, lazima nifanye marekebisho kadhaa lakini pia nitawajenga kisaikolojia wachezaji wangu ili wafanye vizuri katika mechi zilizosalia Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho."

Simba imecheza mechi 20 hadi sasa na kati ya hizo, tisa wamecheza nje ya Dar es Salaam. Timu hiyo ya Msimbazi imebakiza mechi saba kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Mbeya City, Ndanda, Prisons, Toto Africans, Azam, Mwadui na JKT Ruvu na tatu ugenini dhidi ya Coastal Union, Majimaji na Mtibwa Sugar.