Manula kurejea Novemba, Aubin Kramo aanza kutupia

04Sep 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Manula kurejea Novemba, Aubin Kramo aanza kutupia

​​​​​​​GOLIKIPA namba moja wa klabu ya Simba, Aishi Manula anatarajiwa kurejea uwanjani kwenye michezo ya ushindani Novemba, lakini habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kurejea kwa kasi kwa winga wake Aubin Kramo.

Aishi Manula.

Kramo raia wa Ivory Coast aliyesajiliwa msimu huu akitokea Asec Mimosas alikuwa hajacheza mechi yoyote baada ya kuumia mazoezini, lakini jana asubuhi kwenye mchezo wa kirafiki alifunga bao katika mechi ya kirafiki dhidi ya Kipanga ya Zanzibar kwenye uwanja wa Mo Arena, Dar es Salaam.

Tangu atue Simba alikuwa ameichezea timu hiyo kwa dakika 10 tu, akiingia kwenye mechi dhidi ya Power Dynamos kuchukua nafasi ya Kibu Denis dakika ya 80, baada ya hapo hakuonekana tena katika michuano ya Ngao ya Jamii na mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji.

Katika mechi ya juzi, Simba ilishinda mabao 3-0, Kramo akitupia dakika ya 70 kwa mpira wa faulo likiwa ni bao la tatu kwenye mechi hiyo.

Moses Phiri ambaye naye ameanza taratibu kurejea kwenye kikosi baada ya kuwa nje ya dimba kwa muda mrefu kwa majeraha, alitupia bao la kwanza dakika ya 21, huku Luis Miquissone ambaye pamoja na kucheza mechi kadhaa bila kufunga, alianza kufungua akaunti yao ya mabao kwa kupachika bao dakika ya 41.

Mechi hiyo imetokana na programu ya mwalimu Roberto Oliveira ambaye alitaka kikosi chake kupata mechi mbili au tatu za kirafiki kwa ajili ya kuwaweka sawa kwa utimamu wa mwili na pumzi wachezaji wake ambao wamekaa muda mrefu bila kucheza.

Zipo taarifa kuwa huenda Simba ikacheza mechi nyingine dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Wakati huo huo, golikipa namba moja wa timu hiyo,  Manula ameanza mazoezi kwenye Uwanja wa Mo Arena, huku akitarajiwa kuwa anaweza kuwa fiti na kukaa langoni mwezi Novemba.

Manula alionekana jana akifanya mazoezi yake binafsi pembeni, akisimamiwa na madaktari, makocha na watu wa benchi la ufundi ambao walikuwa karibu naye.

Daktari wa klabu hiyo, Edwin Kagabo amesema mchezaji huyo yupo kwenye asilimia 80 kuelekea kwenye 90 ya kupona kabisa.

"Katika matibabu yake tupo kwenye asilimia 80 tunaelekea kwenye 90 ya kuweza kupona kabisa, atafanya mazoezi haya kwa muda wa wiki tatu au nne hivi ili mwili mzima ukiunganisha na sehemu aliyoumia vyote vikae sawa na kuimarisha misuli yote ya mwili, tutegemee mwezi mmoja na wiki moja anaweza kuungana na wenzake kwenye mazoezi," alisema daktari huyo.

Daktari huyo amesema mazoezi anayoyafanya ni awamu ya tatu ya tiba baada ya kufanyiwa upasuaji na kuanza mazoezi tiba na sasa anaendelea na mazoezi hayo lakini ya uwanjani zaidi chini ya uangalizi wa madaktari.

Manula aliumia Aprili 7 mwaka huu katika mchezo wa Kombe la FA kati ya timu yake dhidi ya Ihefu uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ambapo hakumaliza mechi, Simba ikishinda mabao 5-1.