Mkurugenzi Mtendaji ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge, ameyasema hayo, kwenye kambi ya siku mbili ya matibabu bure kwa magonjwa ya moyo na NCDs iliyofanyika katika tawi la taasisi hiyo JKCI-Dar Group, jijini Dar es Salaam.
Amesema wakati taasisi hiyo ikiwa imekwishawafikia wananchi takribani 7,000 kwenye kambi kama hiyo mikoa 11 nchini, wengi wao wamebainika kuwa na tatizo la presha bila kujijua, kutokana na kutokuwa na utaratibu wa kuchunguza afya zao, mara kwa mara.
"Unakuja kutibiwa wakati moyo umekwishatanuka matibabu yake ni ghali, mfano kubadilisha valvu inaweza kufikia Sh. mil 10 hadi 12 kwa upasuaji mmoja. Hivyo ni vyema ukapima afya, ili kama kuna matibabu endelevu ni vyema yatapunguza athari.
"Programu ya Tibamkoba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ni kuwafikia Watanzania pale walipo imewafikia wananchi 7,000 ambao wao tulibaini wanaugua. Zipo sababu kadhaa ambazo zinafanya mtu asifike kwa wakati kupata huduma hospitalini kama za kiuchumi, hivyo mpango huu, unasaidia watu wa kundi hilo," amesema Dk. Kisenge.
Amesema nchini magonjwa ya moyo hasa kwa wagonjwa wanaolazwa hospitalini, yanashika namba tatu ya takwimu ya vifo ikilinganishwa na mengine, kama vile yakuambukiza malaria na Ukimwi, huku duniani magonjwa ya moyo yakigharimu maisha ya watu takribani milioni 17 kila mwaka.
Brigita Boaz, mkazi wa River Side, Ubungo, mkoani Dar es Salaam, amesema iwapo wa kambi hiyo ni muhimu, kwa kuwa husaidia kuwafikia wananchi ambao hawana bima za afya na wenye wenye uchumi mdogo.
"Nimeona bora nije kufanya vipimo katika kambi hii ya bure, hapa imenighatimu nauli tu kuja hapa katika kambi. Nashauri watu wafike, ili kutibiwa iwapo wana shida kiafya," amesema Brigita.









