Man United kumpa mkataba mpya De Gea

03Jul 2023
England
Nipashe
Man United kumpa mkataba mpya De Gea

​​​​​​​KLABU ya Manchester United inapanga mazungumzo ya ana kwa ana na David de Gea katika jitihada za kumbakiza golikipa huyo ambaye mkataba wake umemalizika, vyanzo vimeiambia ESPN.

Mkataba wa De Gea Old Trafford ulimalizika juzi Ijumaa na sasa mlinda mlango huyo ni mchezaji huru.

Anaoa wikendi hii na vyanzo vimeiambia ESPN kwamba United imemruhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka miaka 32 kutumia wakati wake na familia yake nchini Hispania.

Hata hivyo, mabosi wa klabu akiwemo mkurugenzi wa soka, John Murtough wana nia ya kukutana na De Gea ana kwa ana ili kujadili hali ya mkataba wake.

Katika taarifa baadaye siku ya Ijumaa, United ilisema kwamba, mkataba wa David De Gea unakaribia kumalizika, lakini majadiliano yanabaki wazi na kipa huyo aliyekaa muda mrefu.

Kocha Erik ten Hag amesema hadharani anataka Mhispania huyo abaki, ingawa klabu hiyo imekuwa na nia ya kupunguza mshahara wake wa kila wiki wa karibu pauni 375,000 kwa wiki.

United walikuwa na chaguo la kuongeza mkataba wa De Gea kwa mwaka mmoja hadi 2024, lakini waliamua kutoanzisha kipengele hicho.

Vyanzo vimeiambia ESPN kwamba United pia inazungumza na wawakilishi wa Andre Onana kwa nia ya kutoa ofa kwa kipa huyo wa Inter Milan.

Ten Hag anamfahamu vyema mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon baada ya kukaa pamoja Ajax.

Pia kuna nia ya kuwanunua Diogo Costa wa FC Porto na David Raya wa Brentford.

United wameongeza mkataba wa Tom Heaton kwa mwaka mwingine na Dean Henderson amerejea katika klabu hiyo baada ya kukaa kwa mkopo msimu uliopita kule Nottingham Forest.