Makongoro asisitiza ushirikiano kati ya Polisi na Wananchi

20Apr 2023
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Makongoro asisitiza ushirikiano kati ya Polisi na Wananchi

MKUU wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere, amesema hakuna Jeshi la Polisi Duniani ambalo linaweza kuwa na ufanisi bila kushirikiana na jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere (aliyevaa shati jeupe) akiwasalimia wachezaji waliofika finali nyuma yake ni Kamanda wa Polisi mkoani Manyara Kamishna msaidizi wa polisi George Katabazi. PICHA: JALIWASON JASSON

Makongoro amesema hayo leo Aprili 20, 2023 wakati akifunga mashindano ya Polisi Jamii Cup Mjini Babati yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo.

Amesema kutokana na shughuli za kikazi za polisi siyo rahisi wananchi kushirikiana na nao ila kupitia michezo inakuwa rahisi.

Aidha aliahidi kuwa wa kwanza ndani ya miezi sita kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kuungana na jamii inayotoa ushirikiano kwa polisi.

Naye kamanda wa polisi mkoani Manyara Kamishna Msaidizi wa Polisi George Katabazi amesema mashindano hayo yatakuwa endelevu.

Katabazi amesema kupitia mashindano hayo wamepata taarifa za uhalifu zimeongezeka na uhalifu umepungua.

Vile vile amesema wametumia fursa hiyo kupambana na uhalifu kwa kutoa elimu kwa wananchi.

Ametumia fursa hiyo kuwashukru wadau mbalimbali wa maendeleo waliosaidia wakiwemo Kiwanda cha Mati Super Brands Limited kilichopo wilaya ya Babati ambacho kimefadhili michuano hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanan'g Janeth Mayanja, amesema amesindikiza timu yake kutoka Katesh huku akisema wilaya yake timu zote zilishiriki kwenye kata.

Mayanja amesema mashindano hayo yameongeza mahusiano mazuri kati ya polisi na kuondoa woga kwa vijana.

Mashindano ya polisi jamii cup yanahitimishwa leo Aprili 20 zikichuana timu mbili za mpira wa miguu timu ya Katesh kutoka wilaya ya Hanan'g na timu ya Mrara ya Babati.