KMKM FC imefikisha alama 60 huku KVZ FC ikifikisha pointi 59 katika michezo yao ya 27 kila timu iliyocheza zikiwa zimesalia na michezo mitatu kila moja kabla ya ligi msimu huu kumaliza.
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo KMKM, itacheza mchezo wake wa 28 dhidi ya Black Sailor Jumanne katika Uwanja wa Mau majira ya saa kumi alasiri, wakati wapinzani wao, KVZ Alhamisi wakiwa ugenini Kisiwani Pemba dhidi ya wenyeji wao, Chipukizi FC katika Uwanja wa Finya, mechi ikipigwa majira ya kumi alasiri.
Wadau wa soka visiwani hapa wanauangalia zaidi mchezo wa KMKM dhidi ya Black Sailor ambao kila timu inahitaji kupata alama tatu ili kutimiza lengo lake.
Black Sailor inahitaji alama tatu ili kuendelea na harakati za kuepuka kushuka daraja wakati KMKM ikihitaji alama tatu ili kuendelea kuzichanga karata zake za ubingwa wa Ligi Kuu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa KMKM, Ame Msimu, alisema kila mchezo wanaoshuka dimbani wanautazama kama fainali kwao.
Alisema kila mchezo unaumuhimu kwao mpaka ule wa mwisho wa kumaliza ligi, kulingana na msimamo wa ulivyokuwa.
Alisema mchezo wa Black Sailor ndio mgumu zaidi kutokana na kila timu kuhitaji kupata alama tatu kutimiza lengo lake.
“Tumejipanga kupata alama tatu, lakini kama unavyojua ukicheza na timu ambayo inapambania kubaki katika ligi, basi mchezo huwa mkali kwa kuwa mpinzani wetu ili abaki Ligi Kuu anatakiwa ashinde michezo yote, hivyo tunatakiwa kucheza kwa tahadhari sana bila kuharibu mipango yetu," alisema Msimu.










