CAF yabariki Yanga fainali kwa Mkapa

15May 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
CAF yabariki Yanga fainali kwa Mkapa
  • ***Serikali yatoa tamko ikiisubiria kama itafuzu, yatua Sauzi kumaliza kazi, Nabi asema...

WAKATI Yanga wakitua salama Afrika Kusini jana baada ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara juzi, Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), limekubali kusogeza mbele tarehe ya kuanza kufanyika ukarabati katika Uwanja wa Benjamin Mkapa,

Dar es Salaam ili kuipa fursa ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uwanjani hapo endapo itafuzu.

Yanga ambayo juzi ikiwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ilifanikiwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Dodoma Jiji FC mabao 4-2, hivyo kufikisha pointi 74, ambazo haziwezi kufikiwa timu yoyote katika ligi hiyo msimu huu, imetua Afrika Kusini tayari kwa mchezo wao wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Marumo Gallants.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa wiki iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ilishinda mabao 2-0, hivyo keshokutwa, Jumatano itashuka katika Uwanja wa Royal Bafokeng uliopo Rustenberg, Afrika Kusini, ikihitaji sare yoyote ama kutokubali kufungwa zaidi ya bao 1-0 au kupata ushindi wowote ili kutinga fainali.

Na kutokana na Yanga kuwa katika nafasi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho, Caf wametua barua Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuridhia kusogeza mbele tarehe ya kuanza ukarabati mkubwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya michuano ya Super League, ambayo Simba itashiriki, ili kuipa fursa Yanga kuutumia uwanja huo ikiwa itafanikiwa kutinga hatua ya fainali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu, akizungumza na Nipashe jana, alisema walipanga kuufunga uwanja huo mapema mwezi huu, lakini wameamua kusogeza mbele matengenezo hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja zaidi baada ya kukubaliana na CAF kutokana mafanikio ya Yanga kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

"Nataka niwaambie tulikubaliana kuufunga uwanja mwezi huu ili kupisha matengenezo ambayo tumekubaliana ambayo kawaida yanachukua hadi miezi minne.

"Lakini tumeongea na wenzetu wa CAF juu ya suala la Yanga na tumekubaliana kulipeleka mbele kwa kipindi cha mwezi mmoja ili kuacha nafasi ya mchezo wa kwanza wa fainali ikiwa Yanga itafanikiwa kwenda fainali ili ichezwe hapa hapa kabla ya kwenda kwenye mchezo wa marudiano, nafikiria itakuwa ni Juni 3, mwaka huu," alisema Yakubu.

Wakati hayo yakiendelea, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema tayari amewataka wachezaji wake kusahau sherehe za ubingwa baada ya kuifunga Dodoma Jiji FC juzi na badala yake kuelekeza akili zao katika dakika 90 za pili dhidi ya Marumo Gallants keshokutwa, Jumatano.

Alisema mchezo ulikuwa mgumu dhidi ya Dodoma Jiji kwa sababu inapigania kujinusuru kushuka chini na Yanga ikihitaji matokeo mazuri ili kutokuwa na presha kuelekea mchezo wao wa marudiano dhidi ya Marumo Gallants.

“Haukuwa mchezo rahisi wachezaji wamepambana, nawapongeza vijana wangu, watu wangu wa benchi la ufundi, viongozi na mashabiki ambao wamekuwa na sisi kila hatua hadi kutimiza malengo yetu ya kutetea taji letu la ubingwa.

"Hii mechi ambayo ilikuwa muhimu sana kwetu kwa sababu tunahitaji ushindi ili tunapocheza dhidi ya Marumo Gallants tusiwe na presha kubwa juu ya kutetea ubingwa na kuwaza mechi ya nusu fainali ya FA,“ alisema Nabi.

Aliongeza: “Nimeshaongea na wachezaji wangu kwamba furaha na sherehe za ubingwa zimeishia uwanjani na kuwataka kusahau yote, kwa kuwataka kutuliza akili na nguvu zao katika mechi yetu ya marudiano Afrika Kusini”.

Kwa upande wa Rais wa Yanga, Hesri Said, alisema malengo yao ni kuona wanashinda kila mechi, na kwamba hili wamefanikiwa na kwa kutwaa mataji ya Ngao ya Jamii sasa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na sasa wanataka kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na FA Cup.