KMC FC yaiweka Yanga mtegoni ufunguzi Bara

11Aug 2023
Saada Akida
Tanga
Nipashe
KMC FC yaiweka Yanga mtegoni ufunguzi Bara

KOCHA Mkuu wa KMC FC, Abdihamid Moalini, amesema ameridhishwa na utimamu wa mwili kwa wachezaji wake lakini anaendelea ‘kuwasoma’ wapinzani wao Yanga kuekelea mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 15, mwaka huu.

KMC itacheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya bingwa mtetezi, Yanga, Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe, Moalini, alisema anatumia siku chache zilizosalia kwa ajili ya kutengeneza muunganiko wa wachezaji wake kabla ya kukutana na mabingwa hao watetezi katika mchezo huo wa kwanza.

Moalini alisema kikosi chake kilifanya mazoezi mbalimbali ikiwamo ya

utimamu wa mwili, mbinu za ufundi kwa muda wa wiki tatu, jambo ambalo limeimarisha wachezaji wake.

Kocha huyo alisema kazi kubwa aliyonayo sasa ni kuhakikisha nyota wake wanakuwa na muunganiko kwa sababu ya uwapo wa wachezaji wapya na zamani.

“Maendeleo ni mazuri, tumetumia vizuri wiki mbili za maandalizi ya msimu mpya, kwa ajili ya kujenga utimamu wa mwili, sasa bado nafanyia kazi muunganiko, naamini muda wa siku saba zilizobakia tutazitumia vizuri ili kupata matokeo chanya dhidi ya Yanga,” alisema kocha huyo.

Wakati huo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula, alisema baada ya kukamilisha usajili, timu yao iliweka kambi ya muda mrefu mkoani Morogoro.

“Sasa ninavyozungumza tayari kikosi kipo Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Yanga. Kocha Moalini bado ni mgeni lakini tumempa muda kidogo wa kutengeneza timu yake,” alisema ofisa huyo.