Janabi ahadharisha mazoezi bila kupima afya

13Aug 2023
Beatrice Shayo
Dodoma
Nipashe Jumapili
Janabi ahadharisha mazoezi bila kupima afya

MKURUGENZI Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amesema wanaofanya mazoezi ya kukimbia, maarufu kama ‘jogging, wako katika  hatari ya kuanguka na kupoteza maisha gafla.

Prof. Janabi aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2023/24.

Alisema mauti inaweza kuwakuta watu wa aina hiyo kama ambavyo inavyotokea kwenye viwanja vya mpira iwapo watakuwa hawajatambua afya hasa wale wenye ugonjwa wa moyo. Prof. Janabi aliwaomba waandishi wa habari wasiangalie tu wachezaji kuanguka uwanjani.

“Siku hizi kuna ‘j’ogging’ kila mahali nimeona. Ningeomba watu wapime afya zao kwa sababu wale wanaoanguka mpirani na huko ‘jogging’ utaanguka vivyo hivyo,”alisema.

Alikumbushia akiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), michuano ya Kombe la Mataifa la Afrika (AFCON) iliyofanyika Cairo, Misri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipeleka timu ya taifa kufanyiwa uchunguzi na kwamba wachezaji wawili waliondolewa kwa sababu walionekana wanaweza kuanguka uwanjani halafu wakadhani wamelogwa.

Watu hao, alisema walikuwa na matatizo ya moyo kuwa mikubwa na kusema mtu akiwa na tatizo hilo anaweza kuanguka kiwanjani ghafla na kupoteza maisha.

“Wakati nipo mdogo alianguka mchezaji wa Simba na kufariki dunia, anaitwa Hussein Tindwa. Walisema  huyo amerushiwa kitu, hakuna alichorushiwa tatizo ni moyo. Jogging ama GYM (eneo la kufanya mazoezi ya viungo) ni kitu kizuri jambo la msingi ni kupima moyo kabla ya kuingia katika mazoezini.

“Ninashukuru kwa TFF, sijui vyama vingine vya michezo na Baraza la Michezo wanatakiwa kuangalia watu wote wa michezo hasa hii michezo inayotumia nguvu ni muhimu kufanya uchunguzi na hivi vilabu vyetu vikubwa unaingiaje gharama kubwa hujui afya ya mchezaji utalipa mamilioni atakuja siku mbili anakutwa na tatizo la moyo.

“Na jogging tunatakiwa kupima afya zetu, huu ugonjwa unaweza kukukuta upo katika mazoezi,” alisema Prof. Janabi.

Alisema JKCI ina vifaa kamili ya kukagua wachezaji na Hospitali ya Muhimbili imethibitishwa.