Humoud: Sifikirii kurejea Simba

27May 2016
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Humoud: Sifikirii kurejea Simba

MCHEZAJI wa Coastal Union, Abdulhalim Humoud amesema ni bora aende kujiunga na timu za 'mtaani' kuliko kurejea klabu yake ya zamani Simba.

Abdi Kassim kushoto na Abdulhalim Humud kulia wakifanya mazoezi.picha: maktaba.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Humoud alisema hawezi kurejea Simba kwa sababu ni moja kati ya klabu zilizorudisha nyuma maendeleo yake kisoka.

Mchezaji huyo alisema hayo alipoulizwa kuhusu mustakabali wake wa soka baada ya timu yake ya Coastal kushuka daraja msimu huu.

"Yaani hata iweje, siwezi na sitaki kabisa kurudi Simba. Imenifanya nirudi nyuma sana kwenye maendeleo yangu ya soka. Nimerudi kwenye klabu hiyo mara mbili, lakini kuna mambo yanafanyika hayaeleweki," alisema Homoud.

Kiungo huyo ameichezea Simba kwa vipindi viwili tofauti na mara zote ameachwa kwa sababu zinazodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu.

Mara ya kwanza Simba ilibadilishana mchezaji huyo na Azam, ambao waliwapa marehemu Patrick Mafisango, lakini alirejea tena miaka michache baadaye, pia hakudumu kwenye kikosi hicho.