Hukumu ya upangaji matokeo leo

02Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Hukumu ya upangaji matokeo leo

HATMA ya timu itakayopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara kutoka Kundi C itajulikana leo baada ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutangaza uamuzi uliofikiwa baada ya kukamilisha mahojiano.

baraka kizuguto

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF, Baraka Kizuguto alisema jana kuwa kamati hiyo ilitarajiwa kukutana leo asubuhi na mchana itatangaza hatua ilizochukua kuhusiana na 'sakata' la upangaji matokeo uliohusisha timu za kundi hilo.

tff"Kamati itaendelea na kikao kesho (leo) Jumamosi saa 3 asubuhi katika Ofisi za TFF na uamuzi utatangazwa saa 7 mchana," alisema Kizuguto.

Aliongeza kuwa kamati inakutana kwa ajili ya kumalizia shauri la upangaji wa matokeo unaozihusisha timu za Geita Gold, JKT Kanembwa, JKT Oljoro na Polisi Tabora.

Aliwataja viongozi watakaohojiwa na kamati hiyo leo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora) na katibu wake, Fateh Remtullah pamoja na viongozi wa benchi la ufundi la Polisi Tabora; Mrisho Selemani, Boniface Komba na Bernard Rabiamu.

Pia kamati hiyo itamhoji mwenyekiti wa chama cha mchezo huo Mkoa wa Geita, Salum Kurunge na mwenyekiti wa Klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita.