Gamondi avimba droo michuano CAF

27Jul 2023
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Gamondi avimba droo michuano CAF
  • ***Simba yawasubiri Wanamibia au Wazambia raundi ya kwanza kuwania hatua ya makundi...

LICHA ya Yanga kupangwa na 'kibonde' Asas FC ya Djibouti kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikivuka itakwenda kukutana na mshindi kati ya AS Otoho ya Congo dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema analijua soka la Afrika, hivyo aihofii

 

aihofii timu yoyote Shirikisho la Soka Afrika (CAF), jana lilifanya droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, Wawakilishi wa wengine kutoka Zanzibar, KMKM yenyewe itacheza na St. George ya Ethiopia na mshindi wa mchezo huo atakutana na bingwa mtetezi, Al Ahly ya Misri kwenye hatua ya kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi.

Gamondi, aliliambia Nipashe jana kuwa hana hofu ya kukutana na timu yoyote na anaendelea kuiandaa timu yake ili kuweza kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

"Nafahamu kuhusu droo iliyochezeshwa, tumeona wapinzani wetu, lakini niseme tu tunajiandaa kukutana na timu yoyote na hakuna timu tunayoihofia, kikubwa ni kutumia muda wetu vizuri wa maandalizi," alisema Gamondi.

Endapo Yanga itafanikiwa kuwatupa nje Wadjibouti hao watasubiri kucheza na mshindi wa mchezo kati ya AS Otoho dhidi ya El Merreikh ya Sudan kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, Singida Fountain Gate yenyewe itawakaribisha JKU ya Zanzibar katika mchezo wa hatua ya awali na mshindi  wa mchezo huo atakutana na Future Club ya Misri kabla ya kutinga hatua ya makundi.

Azam FC wenyewe wameangukia kwa Bahir Dar Kenema ya Ethiopia katika mchezo wa awali na mshindi wa mchezo huo atakutana na Club Africain ya Tunisia, ambayo msimu ulioisha ilinyoshwa na Yanga katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye michuano hiyo ya pili kwa utajiri barani Afrika.

Michezo ya mkondo wa kwanza kwa hatua ya awali itachezwa kati ya Agosti 18-20 na marudiano itachezwa kati ya Agosti 25-27, mwaka huu.

CAF imefanya marekebisho ya uwendeshaji wa michuano yake ambapo kwa sasa hakutakuwa na faida ya timu inayotolewa raundi ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa kuangukia mchezo wa mchujo wa mwisho wa Kombe la Shirikisho kuwania kutinga hatua ya makundi.

Utaratibu wa sasa timu itakayotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika itakuwa imetoka jumla kwenye michuano ya msimu huu na itasubiri mpaka msimu ujao kama itafuzu.

Msimu uliopita Yanga ilitolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan kwa juma ya mabao 2-1, na kuangukia Kombe la Shirikisho ambako ilifanikiwa kutinga mpaka hatua ya fainali kabla ya kupoteza kwa idadi ya mabao 3-2 mbele ya USM Alger waliotwaa kombe hilo.

Katika droo ya jana, mabingwa hao watetezi wa Kombe la Shirikisho wanasubiri mshindi kati ya AS Loto ya Benin itakayocheza na Fath Union Sport (FUS) ya Morocco kuwania kutinga hatua ya makundi.