Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa kwenye sekta hii ikiwemo kuboreshwa miundombinu ya michezo katika shule mbalimbali ili kuinua sekta hiyo.
Amebainisha kuwa Rais ana dhamira ya kuendelea kuboresha zaidi michezo katika shule zote ili kuhakikisha Taifa linapiga hatua kubwa katika sekta hiyo ikiwemo kuinua vipaji vya wana michezo.
Dk. Mpango amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zozote zinazofanywa na wadau katika kuinua na kuimarisha sekta nzima ya michezo hapa nchini ili kuwezesha wanamichezo kutimiza ndoto zao.
Ili kufikia malengo hayo ameagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha kila shule ya msingi na sekondari inakuwa na mwalimu angalau mmoja wa michezo ili kuimarisha michezo na kuiendesha kitaaluma.
Aidha, amewataka kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanalindwa ili kutoa fursa kwa vijana kupata sehemu za kufanyia mazoezi ya ili kukuza vipaji vyao.
Amesisitiza kuwa maandalizi ya wachezaji mahiri huanza katika umri mdogo hiyo ndiyo sababu ya kuwepo kwa mashindano haya ya Umitashumta na Umisseta ili kuibua mapema vipaji vyao na kuviendeleza.
Dk. Mpango amesema tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassani aingie madarakani ameleta hamasa kubwa kwa wanamichezo na ametenga fedha nyingi ili kuinua zaidi sekta hiyo.
Pia, ameagiza shule zote zinazojengwa kuwa na viwanja vya michezo, kuimarisha na kuboresha usafi wa mazingira ikiwemo kupanda miti kupendesha mazingira yake.
Kwa kutambua mchango na kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua sekta hiyo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hivi karibuni limemtunuku tuzo maalumu ya michezo.
Wakati huo Makamau wa Rais amezipongeza shule za serikali zilizoonyesha uwezo mkubwa na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Ametaja shule hizo kuwa ni Kilombero ya mkoani Morogoro walioibuka mabingwa katika mashindano ya Kanda ya 5 ya Afrika kwa michezo ya mpira wa mikono kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kwa 2023.
Nyingine ni shule ya msingi Mkalapa ya wasichana ya Mkoani Mtwara iliyoibuka kidedea katika mchezo wa wavu kwenye mashindano ya Afrika Mashariki (FEASSSA) yaliyofanyika jijini Arusha Septemba 2022, na shule ya Benjamin Mkapa ya Dar-es-salaam iliyoshiriki mashindano ya soka kanda ya CECAFA.
Makamu wa Rais ameitaka jamii kutambua na kuthamini sekta kwa kuwa ni fursa nzuri ya kupata ajira kwa vijana ikiwemo kutangaza nchi na kukuza sekta hiyo, huku akiwataka wananchi wote kujenga utamaduni wa kushiriki kwenye michezo au kufanya mazoezi.










