Benki ya NBC yazindua kombe jipya la ligi Kuu Tanzania Bara

07Jun 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Benki ya NBC yazindua kombe jipya la ligi Kuu Tanzania Bara

Mdhamini Mkuu wa Ligi ya NBC, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua kombe jipya la Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara lililoboreshwa.

Mkurugenzi wa fedha wa Bodi ya Ligi Ibrahim Mwayela (wa pili kushoto) akilifurahia kombe jipya la ligi kuu ya soka Tanzania bara lililoboreshwa baada ya kuzinduliwa rasmi na mdhamini mkuu benki ya NBC. Wengine katika picha ni wafanyakazi wa NBC benki.

Kombe hilo ambalo lilizinduliwa mbele ya waandishi wa habari leo,litakabidhiwa kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa msimu huu na misimu ijayo.

Akiongea kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa benki ya NBC, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa benki hiyo Godwin Semunyu amesema benki ya NBC ikiwa kama mdhamini mkuu wa ligi imeboresha kombe kutokana na maoni ya wadau mbalimbali wa soka.

“NBC ikiwa mdhamini mkuu wa ligi ya Tanzania bara inajivunia mafanikio makubwa ya ligi yetu. Kwa sasa ligi yetu ni ya tano kwa ubora Afrika nah ii ni hatua kubwa na nzuri kwa soka letu. Leo tumezindua kombe lililoboreshwa ikiwa pia ni sehemu ya kuongeza thamani kwa ligi yetu,” amesema.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa Umma wa benki ya NBC Godwin Semunyu (kulia) akilifurahia kombe jipya la ligi kuu Tanzania bara na mkurugenzi wa fedha wa bodi ya ligi Ibrahim Mwayela (kushoto) wakati wa uzinduzi rasmi wa kombe hilo lililoboreshwa jijini Dar es Salaam.

Godwin ameongeza kuwa, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya ligi, benki ya NBC inatoa bima kwa wachezaji wote wa ligi kuu pamoja na familia zao na pia mikopo ya mabasi kwa timu zinazoshiriki ligi.

“Ili kuongeza hamasa kwa wachezaji na makocha, tunatoa tuzo mbali mbali kwa makundi haya kila mwezi. Benki ya NBC itaendelea kutoa mchango wake katika kusaidia maendeleo ya michezo hapa nchni kwa kuwa inatambua umuhimu na mchango wa michezo  kwa maendeleo,” ameongezea

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa Bodi ya Ligi, Ibrahim Mwayela amesema  udhamini wa NBC umekuwa wenye tija kubwa kwa ligi na kuongeza kuwa NBC ni mdau mkubwa katika maendeleo ya soka hapa nchini.

Muonekano wa kombe jipya la ligi kuu ya NBC litakalokabidhiwa kwa bingwa wa msimu huu na misimu ijayo ya ligi.

"Leo Tanzania tunajivunia ligi yetu kuwa moja katika ligi bora barani Afrika tukishikilia nafasi ya tano. Tunaishukuru sana benki ya NBC kwa udhamini wake ambao umesaidia kufika hapa tulipo huku tukisonga mbele kwa  kujiamini,” ameeleza

Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya NBC wakiwa katika picha ya pamoja na wageni wengine waalikwa wakati wa uzinduzi wa kombe jipya lililoboreshwa la ligi kuu ya NBC Tanzania bara.