Afisa Michezo Mara mgeni rasmi fainali Umoja Cup 2023

17Dec 2023
Na Mwandishi Wetu
RORYA
Nipashe Jumapili
Afisa Michezo Mara mgeni rasmi fainali Umoja Cup 2023

BAADA ya timu nne zilizotinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Umoja Cup 2023 wilayani Rorya kufahamika, hatimaye waandaaji wa mashindano hayo wametangaza rasmi fainali itapigwa mwishoni mwa mwezi huu, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Afisa Michezo wa Mkoa wa Mara, Makondo Makondo.

Katika michezo ya pili ya robo fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na mdau mkubwa wa michezo wilayani Rorya, Peter Owino, ambayo ilipigwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Maji Shirati Sota, Wanamaji FC waliwalowesha Mafundi FC kwa bao 1-0, huku Bubombi  FC wakiwatupa nje ya mashindano Gonga FC kwa mikwaju ya penalti.

Wanamaji FC ambao ndio wenyeji wa mashindano ya Umoja Cup 2023, walifanikiwa kutinga nusu fainali mbele ya mashabiki wao, shukrani zikimwendea nahodha wao, Tumaini Atola, kwa kufunga bao hilo pekee kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya saba ya mchezo.

Mwamuzi wa mchezo huo, Omary Galus, aliamuru mkwaju huo wa penalti baada ya beki wa Mafundi FC, Ooko Wnga, kumchezea vibaya, Nasibu Peter wa Wanamaji FC ndani ya eneo la hatari.

Hata hivyo, mfungaji wa penalti hiyo ya Wanamaji, Atola, alipewa kadi nyekundu katika dakika ya 73 ya mchezo baada ya  kukabana koromeo na mchezaji wa Mafundi FC, Erenest Otieno, ambaye naye alikutana naadhabu hiyo kutoka kwa refa Galus.

Kwa kadi hiyo nyekundu Atola sasa ataukosa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Bubombi FC na ule wa fainali endapo timu yake itafanikiwa kuwatoa Wanamaji FC.

Katika mchezo mwingine wa robo fainali ya mwisho kati ya vijana wa Mpakani, Bubombi FC na wale wa Nyahongo, Gonga FC, ilimalizika kwa mshindi kupatikana kwa njia ya mikwaju ya penalti, baada ya dakika 90 kukamilika miamba hiyo ikitoshana nguvu kwa kufungana mabao 3-3. Katika hatua ya mikwaju ya penalti Bubombi waliibuka kidedea kwa 3-2.

Mwenyekiti wa Mashindano hayo, Ochieng Meli, akizungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki, alisema timu mbili kutoka Kata ya Mkoma Wilaya ya Rorya, Kabwana FC na  Shirati Mji FC, ambazo awali zilitangulia nusu fainali, ndizo zitakazofungua mechi za hatua hiyo katika Uwanja wa Maji Shirati Sota, Alhamisi wiki hii huku Ijumaa nusu fainali ya pili ikipigwa uwanjani hapo pia kati ya Wanamaji dhidi ya Bubombi FC.

Aidha, Ochieng alisema fainali ya michuano hiyo itafanyika mwisho wa mwezi huu, Desemba 31 katika uwanja huo huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa  Afisa Michezo wa Mkoa wa Mara, Makondo.