Biashara United ambayo Ijumaa iliikaribisha Al Ahli Tripoli ya Libya katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kupata ushindi wa 2-0, sasa itahitaji sare yoyote ama kutopoteza kwa zaidi ya mabao hayo watakaporudiana ugenini Jumamosi wiki hii.
Lakini kwa upande wa Azam FC ambayo ililazimishwa sare tasa na Pyramids FC ya Misri katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salam, yenyewe ina mlima mrefu kidogo Jumamosi wiki hii itakapokuwa nyumbani kwa Wamisri hao.
Ushindi ama sare yoyote ya mabao ndivyo vinavyohitajika kwa Azam FC ili kuipa tiketi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa utajiri barani Afrika kwa ngazi ya klabu baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo, timu zitakazopata matokeo ya jumla katika hatua hii, zitasubiri kupangiwa kucheza mechi ya moja ya mtoano nyumbani na ugenini dhidi ya timu zitakazotolewa raundi ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa ili kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Tunatambua haitakuwa rahisi kwa wawakilishi hao wa Tanzania ambao wanahitaji kupata matokeo ili kusonga mbele, hasa ikizingatiwa na ubora wa wapinzani wao.
Lakini tunaamini kama watajipanga vema kuanzia sasa hadi mwishoni mwa wiki kabla ya mechi hizo za ugenini, inawezekana kabisa kwa Azam na Biashara United kupata matokeo chanya na kusonga mbele.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba tayari wamefahamu ubora na udhaifu wa wapinzani wao, hivyo kinachotakiwa ni kufanyia kazi udhaifu wao na kwenda kujitoa kiume mwanzo mwisho wa mchezo.
Kwa Biashara United, inapaswa kutokubweteka kwa matokeo chanya iliyoyapata katika mchezo wa awali nyumbani, na badala yake inatakiwa kwenda kushuka uwanjani ikisaka ushindi kama vile haikushinda awali.
Kadhalika, kwa Azam FC, inafaida kubwa kwa kutokukubali kuruhusu bao nyumbani, hivyo inachotakiwa kukifanya ni kwenda kuhakikisha inauanza mchezo huo kwa kasi na kutafuta bao la ugenini la mapema ili kuwapa wapinzani mzigo mrefu na kuwaongezea presha ya mchezo.
Nipashe hatuna shaka kabisa kwa wawakilishi wetu kwenda kumaliza kazi ugenini endapo tu watafanyia kazi kasoro ndogondogo zilizojitokeza katika mechi zao za awali na kutambua dhamana kubwa waliyoibeba ya kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
Si hilo tu, wachezaji wote wa timu hizo za Tanzania wanapaswa kutambua kuwa hii ni michuano muhimu kwao kwa kuitumia kama daraja la kwenda kutangaza soko lao kimataifa na hatimaye kupata klabu kubwa zaidi Afrika na hata Ulaya.
Hii ni kutokana na michuano hiyo kutupiwa jicho zaidi na mawakala mbalimbali duniani na kila msimu imekuwa tiketi kwa wachezaji wengi kununuliwa na klabu kubwa ndani na nje ya bara la Afrika, hivyo ni wakati wa kila mchezaji kujitoa kufa kupona kwa kutambua yapo maslahi makubwa kwao kwa klabu yao kusonga mbele kwani wanaongeza wigo mpana wa soko lao.










