Fedha za UVIKO 19 utalii zionyeshe tija

19Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Fedha za UVIKO 19 utalii zionyeshe tija

SEKTA ya utalii imepata Shilingi bilioni 90.2 za msaada wa kukabiliana na madhara ya UVIKO 19, kwa ajili ya kuleta mageuzi na kuboresha vivutio vilivyopo na kuongeza vipya ili kupata watalii wengi zaidi.

Athari za UVIKO 19 kwa sekta hiyo zimeonekana kwasababu hutegemea wageni kutoka Ulaya, Marekani, China , India na kwingineko duniani.

Ipo misimu yenye watalii wengi zaidi, kuna kipindi cha msimu wa kati na wastani kulingana na majira ya mwaka lakini pia misimu ya utalii pia hutofautiana kutoka ukanda mmoja wa nchi hadi mwingine.

Kwa Tanzania miezi ya kazi nyingi ni June, Julai, Agosti, Septemba na Oktoba ambacho ni kipindi cha mafuriko ya watalii na fedha nyingi hupatikana wakati huo.

Hivyo Shilingi bilioni 71.9 zitakazotolewa kuboresha sekta ya utalii ziwekezwe kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na UVIKO 19, katika Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka za Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), ile ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Tunashauri fedha hizi zitumiwe kukarabati barabara katika maeneo ya hifadhi za Serengeti, Mkomazi, Tarangire, Nyerere, Kilimanjaro, Saadani na Gombe, eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, misitu 10 ya hifadhi ya mazingira asilia.

Eneo jingine la kutizamwa ni kuweka mfumo wa kielektroniki, kukarabati viwanja vya ndege nane katika hifadhi za taifa za Serengeti, Nyerere,Tarangire, Mkomazi, Saadani na Katavi.

Pia, kujenga malango matano ya kupokelea wageni katika maeneo ya Likuyu Sekamaganga na  Msolwa katika hifadhi za Nyerere, Mkomazi, Mapori ya Akiba ya Swagaswaga na Kijereshi.

Tunaikumbusha serikali kuwa kilio cha kuharibika kwa miundombinu kwenye baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa kimekuwepo hasa nyakati za mvua, kiasi cha watalii kukwama au kushindwa kuvifikia baadhi ya vivutio, hivyo ujio wa fedha hizi ni habari njema na wapenda utalii tunataka kuona mabadiliko.

Kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan, wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano ya UVIKO 19, alitaka fedha hizo kutumika Kwan mujibu wa maelekezo huku akikemea uundaji wa kamati kama namna ya kujipatia fedha hizo.

Watakaopewa majukumu kwakutumia fedha hizo wakumbuke kuwa wananchi wanachotaka ni kuona mabadiliko kwamba sekta ya utalii irudi kwenye mstari na kutoa ajira, kuwezesha mzunguko wa fedha na kuchagiza ukuaji wa maeneo mengine, kwa kuwa fedha hizi ni mkopo ambao kila Mtanzania anayeishi sasa na ambaye hajazaliwa atawajibika kuzilip.

Tunaamini na hatutarajii kuona fedha hizo zinatumika kugharamia shughuli za uendeshaji zaidi badala ya kwenda kwenye miradi na iambayo itaonekana.

Maeneo kama ni barabara zitengenezwe kwa ubora na kupitika kwa kipindi chote cha mwaka na thamani halisi ya fedha ionekane.

Tunawakumbusha waliopewa jukumu la kuisimamia sekta hiyo wakafanyakazi kwa uaminifu na uadilifu ili Watanzania watakapolipa deni wajue zimefanya kazi itakayowanufaisha lao na vizazi vijavyo.

Ni imani yetu kuimarika kwa sekta ya utalii na kuanza kuliingizia taifa fedha ni manufaa kwa kila Mtanzania kwa kuwa mbali na pato kuingia kwenye hazina na kugawanywa kwenye bajeti kuu, l mzunguko wa fedha na ajira kwenye vivutio hivyo utainua maisha ya Watanzania.