Jambo la kusikitisha ni kwamba kauli hizo zinatolewa na viongozi wa kisiasa, ambao wana dhamana kubwa kwa wanaowaongoza na taifa kwa ujumla.
Itakumbukwa kwamba viongozi wa kisiasa wana ushawishi mkubwa kwa wanachama, wafuasi wa vyama hivyo na jamii kwa ujumla, hivyo wanawajibika kuhakikisha kwamba kauli zao na vitendo vyao havina hata chembe yoyote ya kuchochea matukio yanayoweza kuvuruga amani na utulivu nchini.
Wanasiasa wetu wanapaswa kukumbuka kwamba shughuli za maendeleo ya nchi yetu zitafanyika na kuleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla kama tu watahakikisha kwamba amani na utulivu vinaendeleo kuwapo.
Kinyume chake ni kwamba nchi inaweza kuingia katika machafuko ambayo hayatamnufaisha mtu yeyote zaidi ya kusababisha madhara kwa wananchi.
Kwa wiki kadhaa sasa zimekuwa zinatolewa kauli na wanasiasa kuhusu kufanyika kwa maandamano na mikutano ya hadhara katika maeneo yote nchini.
Kauli nyingi zinaonyesha kupaniana na kuonyeshana ubabe, hivyo kuzua hisia kwamba kama vyama vya siasa vinavyolumbana vitafanya maandamano na mikutano hiyo, uwezekano wa kuvunjika kwa amani na utulivu ni mkubwa.
Upande mmoja unasisitiza kwamba utaanza kufanya mikutano na maandamano kuanzia Septemba Mosi na mwingine unasema kuwa utafanya mikutano nchi nzima kuanzia Agosti 31.
Kauli za wanasiasa hao zinaonyesha kwamba wamekosa uvumilivu na ustaarabu wa kisiasa badala yake wametawaliwa na mihemuko, ambayo kamwe haiwezi kuwafanya wakakumbuka wajibu wao wa kudumisha amani na utulivu hususani kuwatuliza wafuasi wao.
Kutokana na hali hiyo, sisi Nipashe tunaona kwamba mchakato mzima wa maandalizi ya maandamano na mikutano iliyopangwa kufanyika kuanzia Jumatano na Alhamisi wiki ijayo siyo sahihi kufanyika katika mazingira ya sasa, ambayo dalili zote zinaonyesha kwamba matukio hayo yatakuwa ya shari.
Badala yake tunashauri kwamba pande zinazohusika zitumie busara kusitisha shughuli hizo na kuketi katika meza ya mazungumzo kusaka suluhu.
Hatuna sababu ya kueleza hoja za kila upande, lakini imani yetu ni kuwa meza ya mazungumzo ndiyo njia pekee inayoweza kuleta maridhiano badala ya kutumia nguvu, ikiwamo mikutano na maandamano.
Hivi karibuni, kuna matukio kadhaa yanayoonyesha dalili za jamii yetu kugawanyika kutokana na sababu za kisiasa.
Baadhi yake ni wabunge wa upinzani kuazimia kutosalimiana na wa chama tawala bungeni, ikiwa ni sehemu ya kumgomea Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
Mgawanyiko mwingine ni wa kisiasa Zanzibar uliosababishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Machi mwaka huu, ambao umesababisha baadhi ya viongozi wa kitaifa wa vyama kutosalimiana, ikiwamo kutopeana mikono.
Ni matumaini yetu kuwa ushauri wetu utazingatiwa na pande zinazovutana na bila shaka wanasiasa hao wanakumbuka athari zilizotokana na maandamano ya kisiasa yaliyotokea Zanzibar Januari 26 na 27 mwaka 2001.
Mgogoro huo haukunufaisha upande wowote, bali kuwaathiri wananchi ambao waliwapoteza ndugu na jamaa zao zaidi ya 30 na wengine kuikimbia nchi kama wakimbizi.
Tunasisitiza kwamba kwa kuwa taifa liko katika vita ya kupambana na ujinga na umaskini, tutanguliwe mbele Tanzania, vyama baadaye.










