Karibu kila mwaka askari polisi wamekuwa wakiuawa wakiwa katika vituo vya polisi, mabemki na kwenye doria kisha kuporwa silaha.
Yako matukio ambayo askari waliuawa na majambazi wakiwa kazini, lakini baadhi ni kwenye benki ya NMB Mwanga mkoani Kilimanjaro na Temeke mkoani Dar es Salaam, kwa kutaja baadhi. Katika matukio hayo, watuhumiwa walikamatwa na kushtakiwa kisha kuhukumiwa.
Kutokana na matukio hayo, Jeshi la Polisi lliliapa kuwa halitakubali kuona vitendo vya mauaji ya askari wake vikiendelea huku likisema wanaovamia vituo vya polisi na maeneo mengine ya doria lengo lao ni kupora silaha kwa ajili ya kufanyia matukio ya ujambazi.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitoa maelekezo kwa Jeshi hilo kutokubali askari wake kuporwa silaha na kwamba wawe wa kwanza kuwanyang’anya silaha majambazi.
Pamoja na hatua hizo, juzi lilitokea tukio la mauaji ya takribani askari polisi wanne na raia wawili katika eneo la Mmbande, Mbagala katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea saa 1:00 jioni wakati askari polisi wakibadilishana lindo la Benki ya CRDB Tawi la Mbande. Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa watu hao waliowahisi kuwa ni majambazi, baada ya kufanya mauaji hayo walitoroka wakiwa na silaha kuelekea kusikojulikana.
Jeshi hilo limethibitisha kutokea kwa mauaji ya askari wake kupitia kwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, na kuwataja waliouawa kuwa ni CPL Yahaya, CPL Hatibu, PC Tito na PC Gastone.
Ingawa Mssanzya alisema tukio hilo la kisasi kutokana na sababu za itikadi za kisiasa, lakini kwa kuwa haijathibitishwa hivyo, bado tunaamini kuwa ni uhalifu kwa kuwa waliofanya mauaji hayo waliwapora askari hao bunduki mbili aina ya SMG na risasi 60.
Watu hao kuua askari na kuondoka na silaha bila kuvunja benki na kuiba fedha isiwe sababu ya kusema kuwa walikuwa wanalipiza kisasi, bali kinachotakiwa kufanyika sasa ni kufanywa kwa uchunguzi utakaosaidia kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo husika ili ukweli ubainike.
Tunasema hivyo kwa kuwa mbinu walizotumia kufanya uhalifu huo zinafanana na wanazotumia siku zote yakiwamo matumizi ya pikipiki na kupora silaha wakati mwingine na fedha kisha kutoweka.
Tunalishauri Jeshi la Polisi kujipanga upya kuhakikisha kwamba matukio ya majambazi kuvamia vituo vya polisi na maeneo mengine ambayo askari wanayalinda yanapatiwa dawa ya kudumu.
Matukio hayo yanasababisha hofu kwa raia pale wanapoona majambazi wanawavamia askari wanaojua mbinu za kujihami na kuwapora silaha na wakati mwingine kuwaua.
Kadhalika, matukio haya yanasababisha hofu kwa watu wanaokwenda katika benki kupata huduma.
Inawezekana zikawapo sababu nyingine zilizosababisha tukio la juzi Mmbande, lakini kinachotakiwa kufanywa na Jeshi la Polisi ni uchunguzi wa kina ili kujiridhisha, badala ya kutoa majibu ya haraka na yenye mwelekeo wa kisiasa.
Suala la msingi ni kuwa tukio la juzi linapaswa kuliamsha Jeshi la Polisi kubuni mbinu na mikakati mipya ya ulinzi wa mabenki, taasisi za fedha na vituo vya polisi kwa kuwa kwa muda mrefu sasa yamekuwa maeneo yanayolengwa na majambazi kwa ajili ya kupora silaha na kuzitumia katika matukio ya ujambazi.










