Tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, alipofuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwa madai kuwa ulikuwa na kasoro nyingi, na kukosolewa na makundi mbalimbali, hali hiyo ndiyo iliyoibua mgogoro mpya wa kisiasa.
Mgogoro huo ulizidi kuongezeka kutokana na hatua ya Jecha ya kutangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi huo, kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na baadhi ya mataifa duniani kupinga hatua hiyo, kwa maelezo kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ulikuwa huru na haki na kwamba ulikuwa bora kuliko wa mwaka 2010, kwa mujibu wa taarifa ya awali ya waangalizi wa kimataifa.
Hatimaye uchaguzi wa marudio ulifanyika Machi 20, 2016, lakini CUF ilisusia kama ilivyoeleza baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa mwaka jana. Hali hiyo ilisababisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda urais na viti vyote vya Baraza la Wawakilishi na udiwani.
Uamuzi wa CUF kususia kushiriki uchaguzi wa marudio ulitoa ishara awali kwamba huo ulikuwa mwisho wa uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoundwa mwaka 2010 baada ya maridhiano yaliyosaidia kurejesha umoja, amani, mshikamano na utulivu wa kisiasa Zanzibar. Dalili za kufa kwa SUK zilitokana na kutokuwapo chama kingine chochote cha upinzani zaidi ya CUF ambacho kina ushawishi kwa Wazanzibari kukipa kura zinazokidhi matakwa ya kikatiba kujumuishwa katika SUK.
Ukweli huo ulidhihirishwa na matokeo ya uchaguzi wa marudio ambao vyama vilivyoshiriki hakuna kilichopata asilimia 10 ya kura zote wala kupata viti vya uwakilishi, hali iliyosababisha CCM ichukue kila kitu na SUK kufa rasmi.
Tumesikitishwa na misimamo inayoendelea kutolewa na viongozi wa CCM na CUF ambao tulitarajia kuwa wanajitafakari upya kukutana kwa ajili ya kutafuta maridhiano ili Zanzibar irejeshe utulivu, amani na umoja vilivyodumu kwa miaka mitano ya uhai wa SUK.
Juzi CUF ilitangaza kutomtambua Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na viongozi wote waliochaguliwa katika uchaguzi wa marudio. Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, ya chama hicho, Twaha Taslima, akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, alisema pia wanaunga mkono vikwazo vinavyoendelea kuchukuliwa kwa kuinyima misaada Tanzania na kwamba hatua hiyo itasaidia upatikanaji wa haki ya kidemokrasia Zanzibar.
Jana, Dk. Shein wakati akilizindua Baraza la Tisa la Wawakilishi, hakutoa kauli yoyote inayotoa matumaini kama yeye na chama chake (CCM) wana mpango wowote wa kurejesha umoja visiwani humo kutokana na mgogoro uliopo.
Badala yake Rais Shein alitoa kauli za jumla za kusisitiza kuwa wao ndio walioshinda, hivyo Wazanzibari wasubiri uchaguzi mwingine wa mwaka 2020 na kwamba mameno yanayosemwa anayasikia, lakini hayamkoseshi usingizi.
Hatufurahishwi na misimamo wanayoendelea kuitoa wanasiasa wa Zanzibar kwa sababu haionyeshi kama wanatambua wajibu na dhamana waliyonayo kwa Zanzibar.
Tunawakumbusha wanasiasa kwamba Zanzibar siyo shwari na njia pekee ya kuinusuru ni pande zote kufikia maridhiano kupitia njia ya mazungumzo huku kila upande ukitanguliza mbele maslahi ya Zanzibar badala ya vyama vya siasa.










