Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipowasilisha Kiwango na Ukomo wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kwa Wabunge wote, akisema kuwa kati ya fedha hizo, mapato ya ndani ni Sh. trilioni 17.79 na kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kukusanya Sh. trilioni 15.1.
Kwa maana hiyo, Serikali italazimika kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwamo kutoza wananchi kodi zaidi ili kufidia pengo la mapato ya ndani ambalo ni takriban Sh. trilioni mbili.
Alisema makusanyo yasiyo ya kodi yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 2.69 huku makusanyo ya halmashauri zote yakiwa Sh. bilioni 665.41 na kwamba serikali inatarajia kupata Sh. trilioni 3.6, ikiwa ni misaada ya wahisani kwenye bajeti kuu ya serikali na miradi mbalimbali wanayoifadhili moja kwa moja.
Kadhalika, serikali inatarajia kukopa mikopo ya masharti ya kibiashara Sh. trilioni 2.1 kutoka vyanzo vya nje na Sh. trilioni 5.37 kutoka vyanzo vya ndani.
Ni kuweli usiopingika kwamba bajeti ya mwaka ujao wa fedha ni kubwa sana kulinganisha bajeti ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Nne ya mwaka wa fedha unaomalizika ambayo ilikuwa Sh. trilioni 22.5, hivyo kuwa na tofauti ya Sh. trilioni saba (7).
Hata hivyo, sababu za msingi za kuongezeka kwa kiasi hicho zinaeleweka kutokana na ufafanuzi uliotolewa na Dk. Mpango jana pamoja na ahadi za Rais John Magufuli, kwamba mipango yake ni kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda.
Pamoja na uwezekano wa bajeti hiyo kuwa chungu kwa wananchi, lakini inatia moyo kwamba serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli, imeonyesha umakini kwa kutekeleza ahadi ya kujikita katika viwanda, kutokana na Waziri Mpango kusema kuwa mwaka ujao wa fedha Serikali imepanga kuiendeleza sekta ya viwanda kwa kuwekeza kwenye ujenzi, kufufua na kuboresha viwanda. Katika mwaka 2016/17, Sh. bilioni 9.3 zitatumika kufufua, kuboresha na kujenga viwanda vipya nchini.
Miongoni mwa viwanda vilivyoingizwa katika mpango huo ni cha Viuadudu cha Kibaha mkoani Pwani, mradi wa Magadi Soda - Bonde la Engaruka mkoani Arusha na mradi wa kufufua kiwanda cha General Tyre – Arusha.
Pia viwanda viwanda vidogo vitaendelezwa katika, mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza. Ziko pia changamoto ambazo kwa namna moja ama nyingine zimechangia kuongezeka kwa bajeti zikiwamo kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani pamoja na wahisani kutotimiza ahadi zao za kuchagia Sh. trilioni 1.09 katika bajeti ya serikali ya mwaka 2014/15.
Pia baadhi ya wahisani kuonyesha kusita kuchangia katika bajeti ijayo. Tunaipongeza serikali pia kwa kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha Sh. trilioni 11.8 (asilimia 40) kwenye miradi ya maendeleo, tofauti na miaka ya karibuni ambako ilikuwa inatumia fedha nyingi katika matumizi.
Ushauri wetu ni kuwa serikali iwe makini katika utekelezaji wa bajeti hiyo kwa kuhakikisha kwamba fedha ilizopanga kuzitumia zinapatikana na zinatumika vizuri kanma zitakavyopangwa hususan kuelekezwa katika miradi ya maendeleo na kuwapo nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.










