Jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alieleza kuwa matokeo ya filamu hiyo yameanza kuonekana na sasa wamepokelewa watalii zaidi ya 700 kutoka nchini Israel, tangu kuzinduliwa mwezi uliopita.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Royal Tour, Dk. Hassan Abbas, alisema hadi jana habari za Royal Tour zimetangazwa kwenye vyombo vya habari zaidi ya 30 na kuwafikia watu milioni 546 duniani, huku 530 walisoma na kusambaza kwa wengine, jambo lililoendelea kuitangaza nchi sehemu mbalimbali.
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Prof. Godus Kahyarara, akizungumza kwenye mkutano wa mtandaoni kuhusu mafanikio ya filamu hiyo, alisema imesukuma mabadiliko ya sera na sheria ambazo zimepitwa na wakati.
Mathalani, alisema sera na sheria nyingi ni za miaka ya 90 ambayo haiko mbali na miaka ya 60, ambazo zilitambua kama kilimo ndicho kitatoa ajira na kukuza pato la nchi huku sekta ya utalii ikiachwa nyuma, hiyo ni kutokana na mazingira ya wakati huo.
Kwa sasa anasema wameona umuhimu kwa kufanya mabadiliko kwa kuwa nyingi zinashindwa kukidhi matakwa ya sasa na hilo limeonekana baada ya kuwapo kwa filamu hiyo na vikao vya mara kwa mara na wadau wa sekta binafsi.
Tunapongeza jitihada zinazofanywa kuhusu Royal Tour kwa kuwa zote zina lengo la kutangaza vivutio vilivyoko nchini duniani, ambavyo vitatembelewa na watalii ambao watatumia muda wao kuwapo nchini, mafanikio ikiwa ni kupata fedha za kigeni zaidi na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Vile vile, itasukuma kufungua fursa nyingine za utalii ambazo hazikuwa zinajulikana na zinaweza kuingiza fedha kwa nchi na mtu mmoja mmoja, kama ambavyo Zanzibar imejipanga kufungua utalii kwenye visiwa vya Pemba ambavyo vilisahaulika.
Ni muhimu serikali kushirikiana na wadu waliopo kwenye sekta ya utalii ambao ndiyo wamewekeza na wanafanya hivyo biashara ya kuuza huduma, ili kujua changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua katika kujiandaa kupokea fursa zinazoletwa na filamu hiyo.
Kwenye utalii kinachouza ni huduma ambayo humfanya mgeni kutumia muda mwingi eneo fulani, ni muhimu kuwafundisha Watanzania namna ya kuyafikia masoko ya bidhaa hiyo duniani, kwa kuwa kumekuwa na madai kuwa kampuni zote kubwa za utalii zinamilikiwa na wageni na nyingi hazijafunguliwa nchini.
Kama ambavyo mwenyekiti wa maandalizi alivyoeleza kuwa Rais alikutana na wadau watano muhimu kwenye sekta ya utalii wakiwamo mawakala wa utalii duniani, mmiliki wa meli za kifahari, majumba ya kuonyesha filamu ambao wote wamejua kilichoko Tanzania na wanaweza kushawishi kutembelea.
Wapo waliokuwa wanaona filamu hiyo haigusi maisha yao kwa namna yoyote, lakini kwa matokeo ya awali yanaonyesha neema kwa nchi ambazo wananchi wanatakiwa kunufaika nazo, maana yake sekta binafsi na wadau wengine wanatakiwa kuwafikia wananchi ili wazione fursa muhimu.
Mathalani, kwenye utalii kuna huduma nyingi zinazoweza kutolewa na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi kama kuuza vyakula na bidhaa nyingine, ni muhimu wakafundishwa namna ya kuzalisha zinazokidhi mahitaji ya soko husika.
Imekuwa kawaida bidhaa au vyakula kununuliwa nje ya eneo husika kwa madai kuwa wananchi hawazalishi kwa viwango vinavyotakiwa, hivyo tunaona ni muhimu wakaelimishwa kuziona fursa na kuzitumia kwa kuwaeleza soko linataka nini.
Ndiyo wakati wa sekta zote muhimu ikiwamo kilimo kuwafikia wananchi kujua matakwa ya soko ili wanapolima wanajua ndicho kinachohitajika, kuliko kampuni za kitalii kuagiza bidhaa au vyakula kutoka nje na kupunguza ajira na fedha kwa mwananchi mmoja mmoja.
Kama ilivyofanyika kwa sekta za gesi wananchi walianza kufundishwa namna ya kuziona fursa na kuzalisha kwa kadri ya viwango vinavyotakiwa, kwa wakati huu wa Royal Tour ni muhimu kunyonya fursa zote ili mwananchi wa kawaida aone umuhimu wa filamu hiyo kwenye maisha yake.
Haipendezi kwamba kwenye hoteli za kitalii mayai, mboga au vyakula vingine vinaagizwa kutoka nje, wakati wananchi wanaweza kufundishwa na kuzalisha kwa ubora unaotakiwa.









