Rais alimpigia simu moja kwa moja na kuzungumza na wamachinga waliohudhuria mkutano wa mafunzo ya viongozi wa machinga (SHIUMA), huku akiahidi ushirikiano na mazingira mazuri ifikapo mwaka huu wa fedha.
Uamuzi wa Rais kutoa fedha hizo ni jambo zuri kwa kuwa watakwenda kuwa na ofisi zinazokidhi mahitaji ya msingi, tofauti na awali ingewachukua muda kuchangishana ili kupata kiasi hicho au ofisi hiyo.
Huenda kwa kuwa na ofisi kutawafanya watambulike kwa maana ya kuwa na rejista ya wamachinga hao kila mkoa, ambayo itasaidia serikali kujua idadi yao na shughuli zao ili wanapotaka kupeleka huduma za kibenki, uwezeshaji na nyingine iwe rahisi zaidi.
Pia itasaidia kuona kama wanakua kibiashara au wanadidimia au inawezekana kuwasaidia wakue zaidi ili kutoka kuwa machinga hadi wafanyabiashara wa kati na juu, ili sasa watoe ajira kwa wengi na kuchangia uchumi wa nchi.
Hadi sasa machinga hawalipi kodi ya mapato inayotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), bali ushuru uliowekwa na halmashauri ambao unatofautiana kutoka eneo moja hadi jingine.
Sisi tunaona ni muhimu kuwa na mipango ya kufuatilia kwa karibu fedha hizo, kwa kuwa uzoefu unaonyesha zimewahi kutolewa fedha kwa makundi fulani lakini ziliishia mikononi mwa wachache.
Mathalani, serikali ya awamu ya nne ya Jakaya Kikwete iligawa Sh. bilioni moja kila mkoa, lakini baadaye ilibainika ziliwafikia wachache na nyingi ziliibwa na wachache ambao walifikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), huku wengine wakiachiwa kwa kukosekana ushahidi.
Fedha hizo zilenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwakopesha, lakini lengo halikufikiwa bali wachache walizitafuna bila huruma kwa wengine.
Kama haitoshi, serikali ikaja na utaratibu wa kila hamashauri kutenga asilimia 10 katika mapato ya kila halmashauri ya mapato yake kwa ajili ya kukopesha wanawake, vijana na wenye ulemavu, lakini wabunge wameeleza namna zilivyopigwa.
Mathalani, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka jana na huu, ilionyesha fedha hizo haziendi kwa wahusika au zilizokwenda hazikurudishwa na sasa kuna madeni makubwa.
Baadhi ya wabunge walisema kuna baadhi ya watumishi wa umma waliamua kukopeshana fedha hizo kwa kivuli cha wananchi, lakini hazikurudishwa jambo ambalo inaonyesha lengo halikufikiwa.
Ndiyo maana tunasema hizi fedha watapewa machinga sawa, lakini ni lazima kuhakikisha zimefika kwenye mikono husika au ikiwezekana wajengewe ofisi na kununuliwa vifaa kwa utaratibu halali na wa wazi usio na urasimu.
Kuzitoa bila mpango maalum zitaishia kuingia kwenye historia kama ilivyokuwa kwenye mabilioni ya JK na makundi maalum ya halmashauri.
Tunatambua fedha hizi zitakaguliwa na CAG kwa kuwa zitatolewa kwenye bajeti ya serikali, hivyo ni lazima kuanza mapema kupunguza mwanya wa kupotea, ili mwakani tusipokee taarifa inayoeleza upigaji.
Pia ni muhimu serikali ikajenga mazingira wezeshi kwa watu kukua kibiashara kuliko kubaki kuwa machinga, lakini kuwatambua maana wapo ambao kwa kuwa wako mtaani wanaonekana wadogo lakini bidhaa walizonazo hawana tofauti na aliye na duka maeneo ya Tandika au Tandale Dar es Salaam.
Lazima kuwe na tafsiri ya machinga kwa kadri ya mazingira yetu na kipimo chake, ili kuepusha nchi kukosa kodi kwa kuwa wengi wanakuwa machinga kwa kuwa hakuna kodi.
Ni muhimu serikali ikafungamanisha shughuli za kiuchumi ili mtu afanye kazi na kupata kipato aliko kuliko kila mmoja kuamini maisha mazuri au ukitaka ‘kutoboa’ lazima uje mjini, ambako wengi huishia kuwa machinga.
Lazima kupanua wigo wa walipa kodi kama chanzo kikuu cha mapato, ikiwa hivyo pamoja na kuziba mianya yote ya wizi nchi itapata fedha za maendeleo yatakayotafisiriwa kwenye maisha ya mwananchi.