Migogoro hiyo iliyoibuka katika miaka ya karibuni, imesababisha mapigano kila uchao baina ya makundi hayo. Kila kundi linalalamikia kuonewa na lingine kuhusu haki ya kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Wafugaji wanaingiza mifugo katika mashamba ya wakulima wakidai kuwa wana haki ya kulisha mifugo yao katika maeneo hayo na wakulima wanadai maeneo waliyomo ni kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Hadi sasa, mamia ya watu wamepoteza maisha sambamba na idadi kubwa ya mifugo. Takribani miezi miwili iliyopita, kundi kubwa la ng’ombe waliuawa kwa madai ya kulishwa katika mashamba ya wakulima huku mtu mmoja akiuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati wa mapigano hayo.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, alifika katika eneo la tukio na kutoa kauli za kulaani kitendo hicho. Nchemba aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi na kuahidi waliohusika kutiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Mapema wiki hii, vitendo hivyo viliibuka tena, baada ya kikundi cha ulinzi wa jadi kinachoundwa na wakulima maarufu kama Mwani, kudaiwa kuvamia nyumba ya mfugaji katika kijiji cha Kambala na kukatakata mifugo takriban 200 wakiwamo ng’ombe, mbuzi na kondoo, kwa kutumia silaha za jadi.
Inadaiwa kuwa wavamizi hao walichukua uamuzi huo kwa lengo la kulipiza kisasi, baada ya mifugo hiyo kudaiwa kula mazao ya wakulima.
Kwa mara nyingine, Waziri Nchemba juzi alifika katika eneo la tukio na kurudia kauli zile zile kwa kulaani vitendo vya kulipiza kisasi na kuiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kuhakikisha waliohusika wanasakwa na kutiwa nguvuni.
Matukio yote mawili ya hivi karibuni, yanadhihirisha kwamba sasa migogoro ya ardhi wilayani Mvomero imekosa mwarobaini, kutokana na viongozi wa serikali kuanzia mkoa hadi mitaa kutochukua hatua za kupata muafaka wa kudumu huku maisha ya raia na mali zao yakiendelea kuwa hatarini.
Yamekuwapo malalamiko kuwa viongozi kadhaa wamekuwa wakihusika na kunufaika nayo ndiyo maana migogoro hiyo haifikii ukomo.
Kauli ya Diwani wa Kata ya Hembeti, Peter Mdidi, aliyoitoa katika mkutano wa kijiji baada ya tukio la wiki hii, kuwa matukio hayo ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yanatokana na uongozi wa wilaya kutotoa ushirikiano na kuwa malalamiko mengi yamekuwa yakifikishwa katika mamlaka mbalimbali bila kushughulikiwa, si ya kubeza.
Tukubali au tusikubali, ukweli unabaki pale pale kwamba Mvomero kuna tatizo na viongozi wenye dhamana serikalini wameshindwa kuwajibika. Hiyo inatokana na ukweli kwamba Nchemba alipata wakati mgumu juzi, baada ya wananchi kugomea kwa muda mkutano wake kwa madai kuwa mkuu wa wilaya amechangia kuendelea kwa mgogoro huo.
Tunashauri kuwa sasa ni wakati muafaka kwa kuwachukulia hatua viongozi wote walioshindwa kuwajibika na kusababisha mauaji ya raia na mifugo katika migogoro ya kila uchao wilayani humo.
Tunaamini kuwa kauli ya Rais John Magufuli kwamba ifike wakati viongozi katika maeneo yenye migogoro ya ardhi isiyoisha waachie nafasi zao kwa wengine.










