Safari njema Yanga, nguvu iongezwe Afrika

10Feb 2016
Mhariri
DAR
Lete Raha
Safari njema Yanga, nguvu iongezwe Afrika

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, wanaondoka leo kuelekea nchini Mauritius kwa ajili ya mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ya huko.

Yanga wanaondoka wakitokea katika matokeo mchanganyiko ya ushindi, sare na kipigo katika mechi tatu zilizopita.

Kabla ya hapo Yanga ilikuwa na kiwango bora kabisa msimu huu ikishinda mechi tano mfululizo na kufunga jumla ya magoli 14 bila ya kuruhusu hata moja.

Matokeo ya mechi tatu zilizopita -- kipigo cha 2-0 ugenini dhidi ya Coastal Union mkoani Tanga, sare ya 2-2 dhidi ya Prison mjini Mbeya na ushindi wa 4-0 dhidi ya JKT Ruvu -- yanamaanisha kwamba Yanga ina uwezo wa kufunga magoli mengi, lakini pia inafungika.

Matokeo ya mechi tano za awali, yangeweza kuwafanya wabweteke wakidhani kwamba ni timu ambayo haifungiki.
Lakini matokeo ya mechi tatu zilizopita ni kengele ya kwao kujitambua umadhubuti wao na udhaifu wao.
Timu kujifahamu udhaifu, ni hatua kubwa sana katika kusaka mafanikio kwenye michuano yoyote, hasa mikubwa kama hii ya Afrika ambayo wanaenda kucheza.

Yanga na miamba wenzao wa soka nchini Simba, wamekuwa katika miaka ya karibuni wakishindwa kuipa umuhimu unaohitajika michuano ya Afrika katika suala la maandalizi na imekuwa ni kawaida kutolewa katika hatua za awali.

Kuwadharau wapinzani ambao hawafahamiki kama miamba ya Afrika kumekuwa kukizigharimu timu zetu, ambazo hazina utaratibu wa kufanya maandalizi mazito kama yale tuliyoyazoea zinapokabiliana zenyewe Simba na Yanga.

Tumezoea kuona maandalizi mazito ya timu zinapokaribia mechi za watani wa jadi hao, kiasi kwamba wakati mwingine wachezaji hufichwa na kunyang'anywa hata simu.

Lakini maandalizi kwa ajili ya kushiriki michuano mikubwa ya Afrika ambayo kwa hakika ndiyo yenye hadhi zaidi na fursa zaidi za kuzitangaza klabu na wachezaji, imekuwa ikikosa kupewa uzito unaostahili.

Miaka 81 tangu kuanzishwa kwa Yanga na bila ya kuwa na mafanikio Afrika, inapaswa kuwa mjadala klabuni. Viongozi, wachezaji na wanachama inapaswa iwaume.

Iwaume kwa sababu kudumaa kwa klabu ni kushindwa kwa uongozi.

Lakini hali hii inaweza kubadilika na mabadiliko yanaweza kuanza sasa wakati Yanga ikienda kuwavaa Cercle wikiendi hii na watakaporudiana baada ya wiki mbili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kila jambo linawezekana, ukitaka lakini.