Wadau saidieni uchunguzi saratani ufikie wengi zaidi

26Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau saidieni uchunguzi saratani ufikie wengi zaidi

JIJINI Dar es Salaam, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, inashirikiana na wadau mbalimbali kuchunguza maradhi ya saratani, lengo likiwa kuwagundua mapema na kuwasaidia watakaopatikana na matatizo.

Kinachochunguzwa ni saratani ya matiti, tezi dume na shingo ya kizazi. Yote haya ni mambo yanayowaumiza watu wengi, kwavile inaelezwa kuwa wanapofika hospitalini kansa inakuwa imeshafikia kwenye hatua za juu na kuongeza hatari zaidi.

Saratani ni ugonjwa unaoweza kuathiri sehemu yoyote mwilini na chanzo chake kinatajwa kuwa ni uharibifu wa seli pamoja na mifumo inayobeba vinasaba (DNA).

Kwa sababu huathiri nasaba inavuruga mpangilio na mwelekeo wa seli zinazogawanyika bila kufuata taratibu za kimaumbile na mara nyingine hugawanyika kabla hazijakomaa na kusababisha uvimbe kutokana na mrundikano kwenye eneo zilipojikusanya.

Saratani hushambulia viungo vingine vya mwili, huingia kwenye mfumo wa damu na kusafirishwa mwilini kwenda sehemu nyingine hatua inayofanya ugonjwa huo kusambaa na kusababisha kifo.

Wataalamu wanasema ukiwahiwa unatibika na pengine kupunguza athari kwa watu wengi, hivyo tunazipongeza kampeni za kuhamasisha wakazi wa Dar es Salaam na kuwachunguza maradhi hayo.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kumekuwa na ongezeko la saratani katika miaka ya kuanzia 2000 na kusababisha wengi kuugua na kupoteza maisha.

Ni wazi Tanzania nayo kama ilivyo sehemu nyingine duniani imeathirika na maradhi hayo.

Takwimu za shirika hilo Afrika, zinaeleza kuwa ugonjwa unaoongezeka na kusababisha vifo.

Tanzania nayo tatizo hilo linatishia maisha ya wengi.

Taasisi ya Ocean Road inaeleza kuwa kansa ya mlango wa kizazi ni tishio kwa kinamama, wakati ya matiti nayo imo. Kadhalika ile ya tezi dume nayo inatishia afya ya wanaume wengi.

Hata hivyo, matatizo ya uharibifu wa mazingira yanachochea uwepo wa jua kali na mionzi yake huongeza uwezekano wa kupata saratani ya ngozi, huku kukiwa na maelezo ya ongezeko la saratani ya ini.

Maradhi haya yasiyoambukizwa yanahusishwa na mabadiliko ya mfumo wa maisha kama kula vyakula vinavyokaangwa na vyenye mafuta mengi, kutumia sukari na bidhaa zenye sukari kupindukia, kutofanya mazoezi, unywaji wa pombe kupindukia na kuvuta sigara vyote vikiumiza mwili.

Maisha yanayohusisha kujamiiana na watu wengi yamekuwa chanzo cha ongezeko la maambukizi ya kirusi cha HPV (Human Papilloma Virus) yanayozidisha saratani ya mlango wa kizazi. Ni kwa kuona ukubwa wa tatizo hili kampeni zinafanyika.

Ndiyo maana tunapongeza juhudi za kuwaelimisha watu wengi na kuwasaidia kwa kutoa elimu na uchunguzi wa bure mara kwa mara ili waweze kutambua dalili za awali za saratani pamoja na kutibiwa.

Lakini kuwapa elimu ya kurekebisha mfumo wa maisha yao ili kujikinga.

Tunaipongeza serikali kwa vile maradhi ni mengi na huenda saratani haijapewa kipaumbele kikamilifu, kutokana na kuwapo magonjwa mengine ya kuambukiza kama malaria, VVU na UKIMWI, magonjwa ya tumbo lakini Tanzania imekuwa mstari wa mbele kupambana na maradhi hayo.

Tunapongeza kampeni za kuchunguzwa watu kutokana na ukweli kuwa asilimia 75 ya wagonjwa hufika hospitalini ugonjwa ukiwa katika hatua za juu na kuwa vigumu kutibika, hivyo kuwahi na kuwachunguza ni kupunguza ukubwa wa tatizo.

Tunaomba taasisi mbalimbali kujitokeza na kushirikiana na Ocean Road, kufikisha huduma hiyo Tanzania nzima.