Unaweza kusema Ofisi ya Msajili kushindwa kukutana na vyama ikiwa ndiyo mlezi wa taasisi hizo za kisiasa unatoa picha kadhaa, kwanza, ni suala la uhusiano wake na wanae hao anaowalea.
Kunahitajika kuwe na uhusiano wa karibu na vyama vya siasa inavyovisimamia.
Pili inahitajika kuwa na ushawishi zaidi wa kuvileta pamoja vyama hivyo ambao ndiyo wadau wake.
Aidha, ushawishi huo ni muhimu ili kuboresha uamuzi ambao umekuwa na lawama kwenye kutafsiri sheria ya vyama vya siasa.
Inavyoonekana ina nguvu kisheria kuamua chochote kile, ikiamua kufanya jambo lolote inalitimiza bila kuzuiliwa.
Hata hivyo, inapaswa kuwa na wepesi kuruhusu mashauriano na vyama hivyo na wadau wengine ili kuwa na maridhiano.
Jambo jingine ambalo ni muhimu kwaofisi hii ni kuanza kuelewa kwa kina uhitaji wa vyama kwa sasa.
Ushauri huu ni muhimu kwavile inavyoelekea vyama kama CHADEMA, ACT Wazalendo na NCCR-Mageuzi vinahitaji kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan na pengine siyo kikao hicho.
Ofisi hiyo imekuwepo kwa miaka mitano sasa ya sintofahamu baina ya vyama na serikali inafahamika. Kinachoendelea kwenye siasa ya vyama vingi nchini na kilio cha mikutano ya ndani kinajulikana.
Ofisi hii ishauriane na wadau mbalimbali ili isimame kutatua changamoto nyingi za vyama vya siasa.
Lakini, pia kuna malalamiko kama ya CHADEMA kuwa viongozi wake wana kesi na wapo mahakamani na wamekosa dhamana na wangetaka waachiwe ili kushiriki mkutano huo.
Kwa hiyo kunahitajika mijadala na mikakati ya kuweka mambo sawa kwasababu ajenda siyo kuzuiwa mikutano ya vyama vya upinzani, hata kesi pia. Wapinzani wanajiona kama majeruhi wa kisiasa.
Waliojeruhiwa kisiasa ni wengi kuanzia walioko mahakamani na magerezani hata vyama vingine kuvurugika.
Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu 2020 umeacha malalamiko na maswali mengi kwenye demokrasia ya vyama vingi nchini.
Ipo haja ya kuwa na mjadala mpana wa kitaifa kuhusu uchaguzi huo hasa kwenye kuwaengua wagombea wa upinzani kwa kutumia sababu nyepesi kama kukosea jina.
Lakini, pia kuna hoja za wabunge wa viti maalumu kuingia bungeni katika mazingira ambayo vyama vinayalalamikia.
Ndiyo maana pengine ni vyema ofisi hiyo ikatafakari zaidi na kuelekeza kipi cha kufanya kwavile kuja na mipango ya kuwakutanisha polisi na vyama vya siasa kunaonekana kuwa ni kukwepa lawama na kuwaangushia polisi jumba bovu la kisiasa.
Taifa lilipiga hatua kubwa miaka michache iliyopita kwenye masuala ya kidemokrasia na uhuru wa kisiasa lakini inavyoelekea linarudi tena nyuma.
Lakini vyama vya siasa navyo vinahitaji kujitafakari na kubadili mikakati yake kwa sasa.
Vikumbuke kuwa kususa mikutano na mlezi wake au Msajili wa Vyama siyo suluhisho kwa sababu majadiliano sio rahisi kuyakwepa kwa mazingira ya sasa.
Ni vyema nao kwenda mstari wa mbele kupambana kushiriki mijadala kwenye kila jukwaa wanalopata au kukaribishwa, walitumie iwe mikutano kama huo ulioitishwa na Msajili wa Vyama.
Vitumie pia vyombo vya habari au kushiriki kwenye uchaguzi wa aina yoyote unaokuja badala ya kulalamika.
Vyama visitegemee huruma za wananchi ambazo hazipo, vishiriki na viwe mstari wa mbele kushirikiana na wananchi, serikali, Ofisi ya Msajili badala ya kususa mambo.