Lengo la ukaguzi ni kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinakuwa na ofisi katika pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa ofisi ya Msajili, pamoja na mambo mengine, mojawapo ya jambo linaloangaliwa kwenye ukaguzi huo ni kukagua ofisi za vyama hivyo Tanzania bara na Zanzibar.
Taarifa ilieleza kuwa ukaguzi na uhakiki wa vyama vya siasa ni takwa la kisheria kuhakikisha vyama vyenye usajili kamili vinatekeleza masharti ya usajili kama yalivyoainishwa kwenye sheria ya vyama vya siasa na kanuni zake.
Hata hivyo, pamoja na Ofisi hiyo kutekeleza takwa hilo la kisheria kwa kufanya ukaguzi na uhakiki wa vyama, baadhi ya wadau wamekuwa wakivilalamikia vyama kadhaa vya siasa kwamba havitekelezi masharti ya usajili, ikiwamo kutokuwa na ofisi zinazoeleweka wala kutofanya shughuli za kisiasa.
Viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakiibuka wakati wa uchaguzi mkuu kuwania udiwani, ubunge na urais, lakini uchaguzi unapoisha hawaonekani tena hadi uchaguzi unaofuata baada ya miaka mitano.
Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inavitaka vyama kuwa na wanachama pande mbili za Jamhuri ya Muungano, lakini kiuhalisia vyama kadha havitimizi sharti hilo baada ya kusajiliwa.
Msajili wa kwanza wa vyama vya siasa baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, George Liundi, alivifutia usajili vyama vya Tanzania People’s Party (TPP) na PONA baada ya kubaini kuwa havikuwa na sifa ya kuendelea kuwapo kutokana na kutofanya shughuli za siasa.
Mrithi wake, John Tendwa, naye hakusita kuvifutia usajili vyama vya CHAUSTA na APPT-Maendeleo, baada ya ukaguzi na uhakiki wa ofisi yake kubaini kuwa vyama hivyo vilishindwa kukidhi masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya Julai Mosi, 1992.
Tunatarajia kwamba Msajili wa sasa, Jaji Francis Mutungi, hatakubali kuviacha vyama vya siasa visivyo na sifa kuendelea kuwapo katika daftari lake baada ya ukaguzi kukamilika katikati ya mwezi huu.
Taifa letu linahitaji vyama vya siasa makini na vinavyokubalika kwa jamii kwa kuwa vina mchango mkubwa katika maendeleo na ndivyo vinavyoshika dola baada ya kupata ridhaa ya wananchi.
Tunaishauri Ofisi ya Msajili katika uhakiki wake ijikite pia kuangalia kama vyama vinafanya mikutano yake mikuu ya uchaguzi kwa mujibu wa katiba zao na viongozi halali waliochaguliwa.
Pia rekodi za wanachama wao kama ni hai, ofisi kama ziko kwenye maeneo rasmi na yanayoeleweka ama kwenye nyumba za watu pamoja na mawasiliano rasmi ya kiofisi kati ya chama husika, taasisi zingine na umma kwa ujumla.
Ni matarajio yetu kuona vyama vinavyobabaisha badala ya kuzingatia matakwa ya kisheria na katiba zao vinachukuliwa hatua stahiki, ikiwamo kufutiwa usajili.
Kwa kufanya hivyo, hatutarajii kama kutakuwapo tena na vyama vya ushaguzi ambavyo huibuka tu unapofika mwaka wa uchaguzi na kuitaka serikali ivipatie ruzuku inayotokana na fedha za walipakodi.










