Miongoni mwa manufaa yatokanayo na hatua hiyo ni kusaidia kuinua kupato cha wakulima wa miti hiyo na serikali kupata kodi. Kuwapo kwa viwanda hivyo pia kunaweza kusaidia kuzalisha ajira kuanzia shambani hadi kwenye viwanda vya kuchakata miti hiyo sehemu mbalimbali nchini, hivyo kuinua uchumi wa Watanzania na taifa kwa ujumla.
Juzi, baadhi ya wakulima wa miti katika mikoa ya Iringa na Njombe, kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili kuwa walianza kukata tamaa na kufikiria kuteketeza mashamba yao ya mikaratusi, kutokana na kukosa soko.
Hata hivyo, wanasema wamesitisha mpango huo, baada ya kuanzishwa kwa viwanda vya uchakataji wa nguzo za umeme kikiwamo kiwanda cha Qwihaya General Enterprises kwenye maeneo yao.
Kwa mujibu wakulima hao, kwa muda mrefu miti hiyo ilikuwa ikilimwa kwa matumizi ya kawaida kama kuni na mirunda kwa ajili ya ujenzi, lakini kwa kuwa thamani yake imeanza kuwa kubwa, baada ya kuwapo kwa viwanda vya kuchakata nguzo za umeme katika maeneo yao, wataendelea kuilima.
Kuwapo kwa kiwanda hicho cha kuchakata miti ya mikaratusi kwa ajili ya nguzo za umeme, tunashauri kwamba iwe ni fursa kwa serikali kuanza kuelekeza nguvu katika kuhamasisha uanzishaji wa viwanda mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Tunashauri hilo, kwa sababu si viwanda vya kichakata mbao tu vinahitajika, bali hata vya kuchakata mazao mbalimbali na matunda ambayo yamekuwa yakiozea mashambani kutokana na ukosefu wa soko.
Tunatambua lengo la serikali ni kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025, ndiyo maana tunashauri uhamasishaji wa kuanzishwa kwa viwanda zaidi hata vidogo vidogo kwa ajili ya kuchakata mbao na hata mazao mbalimbali.
Viwanda vikiwa vingi, tunaamini hata wakulima watalima mazao kwa wingi, kwani watakuwa na uhakika wa sehemu ya kuuza au kuchakata mazao yao na hawatakata tamaa kama ambavyo wale wa mikaratusi walivyotaka kufanya.
Kwa kuwapo uhamasishaji wa kuanzishwa viwanda vingi nchini, tunatarajia kuwa lengo la serikali la kuwa na Tanzania ya viwanda linaweza kuwa matokeo chanya, kwa sababu kwa namna moja au nyingine, kila upande utanufaika.
Viwanda vikianzishwa, vitalipa kodi, wakulipa watalima na wakiuza mazao nao watalipa kodi, viwanda vitakuwa na wafanyakazi, kwa maana kwamba watapata ajira kisha kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa kulipa kodi.
Kulingana na mtiririko huo, ni wazi kwamba, nchi itaendelea kupiga hatua zaidi katika maendeleo kutokana na kodi itakayokusanywa kutoka katika vyao mbalimbali vikiwamo hivyo ambavyo tumevitaja.
Wito wetu kwa serikali ni kwamba ichukulie viwanda vya kuchata miti ya mikaratusi kuwa kichocheo cha kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vingi vya aina hiyo na vya mazao mengine zaidi.
Inawezekana kilimo cha miti hiyo hakiko mikoa ya Njombe na Iringa tu bali na mikoa mingine, ila kikwazo kinaweza kuwa ni sehemu ya kuiuza, ndiyo maana tunashauri kuwapo kwa viwanda vingi zaidi.
Wawekezaji katika viwanda wanaweza kuwa wa ndani au kutoka nje ya nchi, ili mradi Watanzania wafanye shughuli za kilimo wakiwa na uhakika wa sehemu ya kupeleka mazao yao.










