Rais Magufuli alitangaza uamuzi huo akisema kuwa hiyo imetokana na mkoa huo kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusiana na watumishi wa umma hewa. Taarifa ya mkoa huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli kwa wamuu wa mikoa nchini kutakiwa kufanya uhakiki wa watumishi hewa walioko katika mikoa yao na kuwaondoa katika orodha ya malipo ya mshahara (payroll.
Machi 30, mwaka huu wakuu wa mikoa walipowasilisha ripoti ya watumishi hewa katika mikoa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, Kilango alisema mkoa wake haukuwa na watumishi hewa, jambo ambalo ambalo Ikulu Iliamua kulifanyia uchunguzi na kubaini kuwa hadi juzi ilibaini kuliwapo watumishi hewa 45, huku kazi hiyo ikiendelea katika wilaya za Ushetu na Shinyanga.
Akitangaza uamuzi wa kumfuta kazi Kilango, Rais Magufuli alitangaza kusikitisha na sana kwa kuwa tayari Mkoa wa Shinyanga ulikuwa umeshatumia fedha za serikali Sh. milioni 339.9 kuwalipa watumishi hao hewa.
Hatua aliyoichukua Rais Magufuli kama alivyoeleza ni kutokana na kupewa taarifa zisizo sahihi na kiongozi mkuu wa mkoa ambaye alikuwa na wajibu wa kutekeleza agizo la mkuu wa nchi la kusimamia uhakiki, kubaini na kuwaondoa watumishi hewa waliokuwa waliihujumu serikali kwa kuchukua fedha za walipakodi bila kufanya kazi.
Hata hivyo, hatuamini kama Mkuu huyo wa mkoa alitoa taarifa zisizo sahihi makusudi, bali alipotoshwa na watendaji wengine kwa sababu wanazozijua wao, na pengine nao kwa namna moja ama nyingine walikuwa na maslahi katika suala zima la mishahara hewa.
Ndiyo maana inaonekana kwamba kuna mtandao mpana miongoni mwa watumishi wa idara kadhaa za serikali wakiwamo vigogo ambao kwa njia moja wanashirikiana katika kunufaika na fedha za mishahara hewa, na ndiyo sababu wanathibutu kutoa taarifa zisizo sahihi kwa wakubwa wao, wakiwamo wakuu wa mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS) bila kuhofia chochote.
Hatua aliyochukua Rais Magufuli zinapaswa kuwa fundisho kwa viongozi na watendaji wengine wa kuteuliwa; kwamba wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa umakini mkubwa. Kiongozi anapopewa taarifa kutoka kwa walioko chini yake kufanya jitihada za kujiridhisha kama taarifa hizo zina ukweli ndani yake, badala ya kuichukua kama ilivyo na kuiweka hadharani au kuiwasilisha kwa mamlaka ya juu zaidi.
Funzo lingine kwa viongozi na watendaji wa serikali ni kwamba wakati huu wa kuitumikia serikali ya awamu ya tano wanapaswa kubadilika kimitazamo (mindset) ili waende na kasi yake kama rais Magufuli anavyosisitiza mara kwa mara.
Kilichofichuka Shinyanga ni uthibitisho kuwa kuwafichua watumishi hewa ni vita ngumu ambayo inahitaji uthubutu ili kuishinda, kwa kuwa kuna watu ambao wamejipanga kwa kutumia kila mbinu kuhakikisha kwamba wanaendelea kunufaika kwa kuchukua fedha ambazo hawakuzitolea jasho.
Tunawashauri viongozi na watendaji wote waliopewa dhamana ya kusimamia jumumu hilo wanashirikiana na kuhakikisha kwamba taarifa wanazopewa na walioko chini yao wanazifanyia kazi kwa kina na kujiridhisha kuwa zina ukweli ndani yake pamoja na kujiepusha wasije kutoa taarifa zisizo sahihi kwa mamlaka za juu akiwamo Rais Magufuli.










