Utouh anaheshimika nchini kutokana na alivyoibadili ofisi ya CAG na kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi, anasema kuwa hatua zinazochukuliwa kwa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kudhibiti tatizo hilo siyo mwarobaini na kwamba ni vigumu kukosekana watumishi hewa kwa mfumo uliopo.
Utouh ambaye alihudumu kwenye nafasi ya CAG kwa miaka minane mfululizo na ofisi hiyo kufichua madudu mengi ya ufisadi serikalini, aliliambia Nipashe katika mahojiano juzi yaliyochapishwa katika toleo letu la jana kuwa, tatizo la watumishi hewa lina sura mbili ambazo zinatakiwa kushughulikiwa na serikali ya awamu ya tano, akizitaja kuwa ni uzembe na mfumo mbovu wa uajiri kwenye sekta ya umma.
Alisema ni lazima jitihada za serikali zielekezwe katika kuchimbua kiini cha watumishi hewa na kulishughulikia kwa kuwa bila kufanya hivyo, baada ya miezi sita wataibuka tena.
Alisema sababu moja inayosababisha watumishi hewa ni uzembe, kwa sababu kama mtumishi akifariki duniua, ofisi inapata taarifa na wanashiriki kwenye maziko, lakini wanasahau kutoa jina lake na lignin ni mfumo mbovu. Kwamba mtumishi anapoajiriwa, anaandika taarifa zake zote ambazo zinaonyesha ni lini atastaafu, hivyo ilitakiwa kuwapo mfumo ambao k unaweza kutoa ujumbe wa kustaafu na ambao utamuondoa kwenye utumishi moja kwa moja, lakini hilo halifanyiki.
Kwa mujibu wa Utouh, tatizo lingine la watumishi hewa linatokana na mtandao wa watu kadhaa ambao wananufaika na mishahara hiyo na kutolea mfano wa mtumishi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye alikuwa analipwa mshahara zaidi ya mmoja na kuongeza kuwa isingewezekana kupata malipo hayo kama idara ya uhasibu pamoja na utawala kutofahamu jambo hilo.
Utouh alibainisha mambo mengi, lakini kubwa zaidi kauli yake imefanana na msimamo wetu ambao tumeutoa mara kadhaa kwamba kuna wanainufaika na mishahara hewa kutokana na wahusika kuzigawana fedha hizo.
Kwa ujumla tunakubaliana na CAG huyo mstaafu kwamba mfumo uliopo siyo mzuri kwa ajili ya kudhibiti watumishi hewa, hivyo kuna haja ya kuuangalia upya ili iwe rahisi kuwatambua mara moja na kuwaondoa katika orodha ya malipo ya mshahara watumishi wanaostaafu, kufariki, kuacha kwazi kwa hiyari yao au kuondolewa katika utumishi.
Ni jambo lisiloingia akilini mtumishi kufariki, kufukuzwa, kuacha kazi mwenyewe au kustaafu na akaendelea kulipwa mshahara kwa miaka kadhaa wakati wakubwa wake wa kazi kuanzia mkuu wake wa kitengo, idara wanazo taarifa.
Swali la kujiuliza hapa ni je, hao hawapeleki rasmi taarifa hizo na kwa wakati katika idara za uhasibu na utawala? Jibu la haraka hapa ni kwamba utendaji katika idara hizi unatia shaka na ndio unaoibua hisia za wengi kuwa baadhi ya watumishi wake wanahusika moja kwa moja na mtandao unaoihujumu Serikali kwa kuacha majina hayo na kuendelea kujinufaisha kwa mishahara yao.
Tunaunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na suala la watumishi hewa na ushauri wetu ni kwamba iufanyie kazi ushauri uliotolewa na Utouh kwa kuwa suala hilo analijua vizuri kutokana na uzoefu wake wa miaka minane aliyoitumikia nafasi ya CAG.










