Wiki iliyopita tuliandika maoni tukizitahadharisha mamlaka zinazohusika kuhakikisha kwamba zinamaliza kwanza kero zilizobainika wakati wa siku za majaribio ambazo mabasi hayo yalikuwa yanasafirisha abiria bila malipo kuanzia Mei 10 hadi juzi.
Changamoto kadhaa ambazo zilibainika katika siku za majaribio ni baadhi ya wenye magari binafsi, pikipiki na daladala kupita katika barabara za mabasi ya mwendokasi wakiwa wamebeba abiria.
Jana changamoto zilizobainika ni utaratibu wa tiketi za elektroniki kutowatambua askari polisi ambao awali walikuwa wanasafiri bure katika daladala pamoja na walimu waliokuwa hawalipi nauli wakati wa kwenda kazini na kurudi.
Pia, baadhi ya wakazi mfano, wa Mbezi jana walijikuta wakilipa nauli ya Sh. 1,050 badala ya nauli elekezi ya Sh. 800 kutokana na mfumo wa risiti zinazokatiwa Mbezi mwisho, kutosoma katika mfumo wa kukagulia risiti kabla ya kupanda mabasi hayo katika kituo cha Kimara mwisho, hivyo wakazi wanaotoka Mbezi kwenda Kimara mwisho kulazimika kupanda mpaka Kimara mwisho kwa nauli ya Sh. 400 na kukata tiketi nyingine za kwenda mjini kwa Sh. 650.
Kadhalika, abiria walitumia muda mrefu takribani dakika 20 kukata tiketi za mabasi ya mwendokasi huku wakitozwa kati ya Sh. 700 hadi 800 badala ya 650 kutokana na ukosefu wa chenji.
Aidha, mawakala wa kukatisha tiketi walichelewa kufika vituoni, hali iliyowasababishia usumbufu wakazi wa maeneo mengi waliofika kituoni Mbezi alfajiri kuwahi mabasi hayo.
Katika baadhi ya vituo, abiria walishindwa kupanda mabasi hayo kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme inayowezesha ukataji wa tiketi za kupanda mabasi hayo. Vile vile, katika baadhi ya vituo vya mabasi hayo, abiria walipanga foleni kusubiri huduma ya ukataji wa tiketi kutokana na mashine kuchelewa kutoa taarifa.
Changamoto nyingine zilizosababisha usumbufu ni kukosekana kwa kadi, tiketi kuharibika baada ya saa mbili, tiketi kutokuonyesha bei ya nauli na kukosekana kwa huduma za vyoo.
Kwa mara nyingine tunashauri kwamba mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua za haraka baada ya kubaini changamoto zinazojitokeza hususan za jana.
Kuendelea kutokea changamoto mpya kama za jana ni ishara kuwa hapakuwapo na maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza rasmi utekelezaji wa mradi huo.
Ukiangalia changamoto hizo zote utaona kuwa sababu kubwa ni wahusika kutofanya maandalizi ya kutosha. Kwa mfano, masuala ya kukosekana kwa chenji na nauli kutoonekana kwenye tiketi yalikuwa ndani ya uwezo wao.
Ni kitu kisichoingia akilini kukosekana kwa vyoo wakati wakati ni suala ambalo lilitakiwa kukamilishwa kabla ya mabasi kuanza kutoa huduma.
Ndiyo maana tulitahadharisha kabla kwamba kama wahusika wa mradi wataona kuwa maandalizi hayajakamilika, wasione aibu badala yake waongeze muda wa majaribio ili safari zikianza pasiwepo usumbufu kwa abiria na umma kwa ujumla.
Tunaamini kuwa changamoto zilizojitokeza jana zitatoa fundisho kwa wahusika kwamba wanawajibika kuzitafutia ufumbuzi haraka ili kumaliza usumbufu huo.
Tunasubiri kuona watekelezaji na wasimamizi wa mradi huo, Uda-Dart wakirekebisha kasoro zote zilizotokea au watangaze kusitisha huduma hiyo wakati wakiendelea kuweka mambo sawa, vinginevyo watu wataanza kuwatilia shaka.
ends










