Habari hizo zilieleza kwamba pamoja na msichana huyo kufanyiwa vitendo hivyo na kundi la wamaume zaidi ya 10, watu hao pia walimpiga picha ya video akifanyiwa udhalilishaji huo na kuituma katika mitandao ya kijamii ambayo pia mama yake mzazi aliiona kupitia simu yake ya mkononi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, mbali na kuthibitisha kutokea kwa tukuo hilo, alisema kuwa watu hao pia walimtishia msichana huyo kwa kisu kuwa akikataa kufanya nao mapenzi, wangemuua na vile vile kumwambia kuwa asithubutu kutoa siri hiyo kwa mtu yeyote.
Kitendo hicho kimetusikitisha sana na bila shaka jamii nzima ya Watanzania watakuwa wamekillani kutokana na kudhalilisha utu wa binadamu. Malengo ya watu hao kumdhalilisha binadamu mwenzao hayaeleweki.
Kama msichana huyo aliwafanyia kosa, walipaswa kumpeleka katika vyombo vya sheria, badala ya kujichukulia sheria mkononi, tena kwa kumfanyia kitendo cha ukatili na udhalilishaji, ambacho kimeitia aibu jamii nzima.
Hatuelewi ni sababu zipi zilizowafanya wahalifu hao kumpiga picha za video na kuzisambaza kwa watu wasiohusika, akiwamo mama yake mzazi. Kitendo hicho kinakwenda kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mitandao ya 2015.
Sheria ya Mkosa ya Mitandao pamoja na kupingwa na makundi kadhaa katika jamii kwamba inaingilia uhuru binafsi na uhuru wa kutoa maoni, lakini moja ya umuhimu wake ni kuwadhibiti watu wanaoitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kufanya vitendo ambavyo vinadhalilisha watu wengine na vinavyokiuka maadili.
Kitendo hicho kinadhihirisha kwamba kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii yetu na linatupatia changamoto ya kuchukua hatua madhubuti za kukomesha vitendo vinavyokwenda kinyume cha maadili ya jamii.
Miongoni mwa hatua za kuchukua ni kutungwa kwa sheria kali zaidi dhidi ya wanaofanya vitendo vya ukatili na udhalilishaji, lakini pia taasisi kadhaa zinazojihusisha na kutetea haki za wanawake na watoto kikiwamo Chama cha Waandishi Wanawake Tanzania (Tamwa) ziendelee kuihamasisha jamii kupambana na vitendo ukatili na udhalilishaji wa kijinsia na kuchukua hatua ikiwamo kuyaripoti matukio hayo kwa vyombo vya dola ili wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Tunalipongeza Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa kuchukua hatua haraka na kuwakamata watuhumiwa 11 wa tukio hilo baada ya mwathirika kuriripoti.
Kuna watu kadhaa ambao wanakumbwa na matukio ya udhalilishaji kama hili, lakini kutokana na kukutokuwa na uelewa wa kutosha au aibu wanaamua kukaa kimya bila kuripoti Polisi.
Tunawahimiza kuyaripoti matukio hayo kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuwafanya wahalifu waogope kutenda makosa hayo yanayodhalilisha utu.
Kwa kuwa Jeshi la Polisi limewatia mbaroni baadhi ya watuhumiwa, tumaanini kuwa sheria itachukua mkondo dhidi ya watakaokutwa na hatia kuhusiana na tukio hilo.
Licha ya baadhi ya mashirika ya haki za binadamu na ya kutetea haki za wanawake nchini kutoa matamko ya kulaani kitendo hicho, lakini tunayashauri yasiishie hapo, bali kuendelea kufuatilia kesi hiyo katika vyombo vya sheria ili ishughulikiwe haraka.










