Uchangiaji ujenzi madarasa ni jukumu la wote

08Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uchangiaji ujenzi madarasa ni jukumu la wote

DESEMBA 18, mwaka jana serikali ilitoa agizo kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa unakuwa endelevu kwa sababu idadi ya wanafunzi walioandikishwa na wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza inafahamika.

Iliagiza ifikapo Februari 28, mwaka huu ujenzi wa vyumba vya madarasa uwe umekamilika na kuwezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaingia darasani.

Kila halmashauri imetakiwa kujenga vyumba vya kutosha vya madarasa kuondoa adha ya wanafunzi kukosa nafasi ya kuanza masomo kutokana na ukosefu wa vyumba hivyo.

Akitoa agizo hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitaka kila mtoto wa Kitanzania aliyefaulu aende sekondari na jukumu la halmashauri ni kuhakikisha inajenga vyumba vya kutosha vya madarasa na walimu waendelee kufanyakazi kwa bidii kwa kuwa serikali inatambua na kuthamini kazi nzuri wanayoifanya ambayo inawezesha kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofaulu kila mwaka.

Katika kutekeleza agizo hilo wadau mbalimbali wa elimu wamejitokeza kuisaidia serikali kukamilisha lengo hilo ili kila mtoto aliyefaulu kujiunga na sekondari asikose nafasi hiyo.

Mashirika, kampuni, watu binafsi, taasisi, viongozi mbalimbali wa kisiasa na kiserikali ni baadhi tu ya wadau wa elimu walioamua kujitoa kuisaidia serikali kutimiza lengo hilo la kila mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na sekondari asikose nafasi hiyo.

Misaada hiyo ni pamoja na vifaa vya ujenzi, fedha taslimu na nguvu kazi.

Moyo huu wa kujitoa wa mashirika na taasisi mbalimbali uwe chachu ya kila mwananchi kujitoa kuchangia ujenzi huo wa vyumba vya madarasa.

Juhudi hizo zisipofanikiwa watoto watakaokosa nafasi ya kuingia darasani kwa kukosa vyumba, wataachwa katika mazingira hatarishi.

Ndoto yao ya malengo waliyojiwekea itakuwa imezima na kuwaathiri kisaikolojia na wengine kujiingiza katika mambo yasiyofaa.

Wapo wananchi wanaojitoa kuchangia ili kutimiza malengo ya watoto wao, lakini kuna baadhi wanakwamisha kwa kutumia michango hiyo kuitafuna kwa manufaa yao.

Katika tukio moja lililoripotiwa juzi, kuna baadhi ya kamati zilizoundwa kusimamia makusanyo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuamua kutafuna fedha hizo, hali inayorudisha nyuma ari ya wananchi hao kuchangia.

Ikumbukwe kuwa ujenzi huo utanufaisha pia vizazi vijavyo ambao utanusuru wimbi la watoto wanaobaki mtaani na kujiingiza katika makundi ya kihalifu.

Tukumbuke miaka ya nyuma wakati watoto walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi ilikuwa ni kipindi cha mawakala cha kuwatafuta na kuwapeleka kutumikishwa kazi za ndani.

Serikali kwa sasa imeondoa tatizo hilo kwa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya bure na hiyo imesababisha watoto wengi kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari hali inayofanya kuwapo na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa sababu ya idadi kubwa ya watoto wanaochaguliwa.

Ushirikiano unaoonyeshwa na wadau mbalimbali uungwe mkono kutimiliza lengo la kila mtoto aliyechaguliwa kuingia sekondari anapata nafasi.