Simba, Namungo muda wa kupambana umefika

09Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Namungo muda wa kupambana umefika

KWANZA tunapenda kutoa pongezi kwa wawakilishi wa Tanzania ambao wanashiriki katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ya jijini Dar es Salaam kwa kufanikiwa kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Simba iliyokuwa chini ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck (ameachana na timu hiyo juzi), pamoja na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Suleiman 'Veron' Matola imetinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga FC Platinum kutoka Zimbabwe jumla ya mabao 4-1.

Hii ni baada ya kupoteza katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini Harare kwa kufungwa bao 1-0, lakini Jumatano iliyopita ikatoa kipigo kitakatifu cha magoli 4-0, kwa wapinzani wao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Kwa matokeo hayo, Simba imeungana na timu nyingine 11 kutoka katika nchi mbalimbali barani Afrika kucheza hatua ya makundi, baada ya msimu uliopita wa mashindano hayo kutolewa mapema na UD Songo ya Msumbiji.

Mbali na Simba, wawakilishi wengine wa Tanzania waliobakia kwenye michuano hiyo ya kimataifa ni Namungo FC kutoka mkoani Lindi ambayo pia imefanya vyema kwa kuwaondoka Al Hilal Obeid ya Sudan kwa jumla ya mabao 5-3.

Namungo iliwafunga Wasudan hao mabao 2-0 katika mechi ya kwanza hapa nyumbani na ikalazimishwa sare ya mabao 3-3 walipokuwa ugenini jijini Khartoum.

Mechi hizo zimemalizika na sasa hivi Simba na Namungo zinatakiwa zijiimarishe kuelekea hatua inayofuata katika michuano hiyo inayosimamiwa na kuandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Simba na Namungo zinatakiwa kupitia mapema ripoti zao za kiufundi na kutumia muda mdogo wa usajili uliobakia kuimarisha vikosi vyao ili watakaposhuka tena uwanjani wawe tayari kushindana na si kushiriki kama ilivyozoeleka.

Usajili mzuri na utakaofanyika kwa malengo, utazisaidia timu hizi mbili kuwa na vikosi imara ambavyo vitatoa matokeo mazuri na hatimaye nchi kuweka rekodi ya kushinda mataji hayo yanayowaniwa na wawakilishi wetu hao.

Timu hizi mbili zitakapokuwa na vikosi imara, zitajiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo chanya katika michezo yake iwe nyumbani au ugenini na kulitangaza vyema jina la Tanzania kwa upande wa soka.

Umefika wakati, timu za Tanzania zinapopata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa zikaogopewa kila zinapoonekana kwenye michuano hiyo na kamwe zisiwafanye wapinzani wao kuwaona 'ni wa kawaida'.

Inafahamika wazi katika mchezo wa soka hakuna kutegemea miujiza, inaeleweka ili timu yao ivune matokeo mazuri ni lazima wahusika wakubali kuwekeza kwa kufanya usajili wa kiwango cha juu, kuandaa programu sahihi ya kambi pamoja na kuwapatia wachezaji mahitaji yao yote muhimu.

Mataji au mafanikio yoyote kamwe hayapatikani kwa miujiza bali hutua kwenye timu iliyojiandaa vyema kuanzia hatua ya mwanzo wa msimu au ile iliyotumia vizuri kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Kuendelea kufanya vyema kwa klabu hizi, kutaihakikishia zaidi Tanzania nafasi ya kuwakilishwa na timu nne kwenye michuano hiyo kwa sababu ya idadi ya pointi itakazovuna.

Hakuna kisichowezekana, timu hizi mbili zinatakiwa kuendelea kujipanga kwa sababu hatua ambayo wamefika ni muhimu na kila klabu inahitaji kufika huko.

Viongozi wasiangalie wanatakiwa kutumia kiasi gani, wawekeze kuimarisha vikosi vyao kwa sababu mwisho wa siku, watavuna neema kupitia zawadi itakayotolewa na CAF.