Bila kuuma maneno, IGP Sirro aliweka bayana kwamba baadhi ya askari wa kikosi hicho, wamekithiri kwa vitendo vya rushwa ambavyo vimelitia doa jeshi hilo katika ya Watanzania.
Sirro katika taarifa yake hiyo alisema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa watu wenye magari kwamba askari wa kikosi hicho wamekuwa wakiomba na kupokea rushwa, hatua ambayo imekuwa kero kwao na upande mwingine inalitia doa jeshi hilo.
Moja ya njia ambazo askari hao wamekuwa wakitumia kujihalalishia rushwa ni kuwasimamisha kwa muda mrefu madereva na wenye magari kwa makosa madogo madogo bila sababu za msingi.
Kutokana na hali hiyo, alisema jeshi hilo limejipanga kumaliza tatizo hilo na njia mojawapo katika kufikia azma hiyo ni kubaini askari wanaojihusisha na kuomba rushwa na kuwachukulia hatua.
Moja ya mkakati katika kupambana na tatizo hilo, kwa mujibu wa kiongozi huyo mkuu wa polisi, ni mabadiliko ambayo yamefanywa ndani ya kikosi hicho kwa kuteua kamanda mpya. Alisema mkuu huyo wa trafiki, Wilbroad Mutafungwa, ameshapewa maagizo namna ya kulishughulikia tatizo hilo.
Sambamba na hatua hiyo, Sirro alisema wataendelea kutoa elimu kwa askari na wananchi kupitia vikundi vya ulinzi shirikishi na kutumia vyombo vya habari.
Hatua ya IGP Sirro ya kuweka bayana vitendo vinavyofanywa na askari ili kuhalalisha rushwa, inaonyesha dhahiri kwamba amedhamiria kuchukua hatua stahiki baada ya kuwapo malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, huku baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa jeshi hilo wakiwakingia kifua wahusika.
Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kwamba askari hao wanafanya hivyo kwa kutumwa na baadhi ya wakubwa wao wakiwamo maofisa wa usalama barabarani wa mikoa na taarifa zinaopowafikia wanakuwa wakali kwa wananchi.
Ni ukweli kwamba baadhi ya askari wa usalama barabarani wamekuwa vinara katika kulipaka tope Jeshi la Polisi kutokana na kuendekeza rushwa. Baadhi ya askari hao, kama alivyosema IGP, wamekuwa wakijificha kwenye vichaka au sehemu ambazo si rahisi kubainika kuwa wanapokea rushwa.
Katika barabara za mikoani kama kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Tanga, kuna maeneo kadhaa ambayo wametengeneza vijiwe kwa ajili ya kuwasimamisha madereva kwa madai ya kukagua au kudai kwamba wamezidisha mwendo. Lengo kubwa la kufanya hivyo ni kutaka rushwa.
Kama alivyosema IGP vitendo vya rushwa ndani ya Jeshi la Polisi vinapaswa kufika mwisho. Njia muhimu katika kufikia hilo ni maofisa wa juu wa polisi kutoa namba zao ili wananchi wanaoathirika na vitendo hivyo watoe taarifa kwao. Polisi bila rushwa inawezekana.










